TFNC YAENDESHA ZOEZI LA JARIBIO LA AWALI LA UJUMBE WA PICHA KUHAMASISHA WA LISHE KWA WANAFUNZI

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Esther Nkuba akiwaonesha picha ya uhamasishaji kula vyakula mchanganyiko wanafunzi wa Shule ya Msingi Charambe wakati wa zoezi la kufanya jaribio la awali la ujumbe na picha za uhamasishaji wa masula ya lishe kabla ya kuanza kutumika katika mradi wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule za msingi 15 za Manispaa ya Temeke.

Mradi huu unatekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Manispaa ya Temeke na TFNC.

*************

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na Manispaa ya Temeke imeendesha zoezi la jaribio la awali la ujumbe na picha za uhamasishaji wa masuala ya lishe kwa wanafunzi, walimu na wazazi wa shule za msingi Manispaa ya Temeke.

Akiongea wakati wa zoezi hilo lililofanyika katika Shule ya Msingi Charambe, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka TFNC, Dkt. Esther Nkuba amesema kuwa zoezi hilo linafanyika ili kukusanya maoni kutoka kwa walengwa yatakayosaidia uboreshwaji wa nyenzo za kufikisha elimu ya lishe katika utekelezaji wa mradi wa afya na lishe shuleni.

“Mradi wa afya na lishe shuleni unatekelezwa katika shule za msingi 15 ndani ya manispaa ya Temeke unaolenga kufanya uhamasishaji na kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula wakiwa wapo shuleni”

Aidha Dkt. Nkuba amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha watoto wenye umri wa shule wanakuwa na lishe bora ikiwemo utungaji wa mwongozo wa kuwapatia watoto chakula shuleni.

Dkt. Nkuba amesema licha ya jitihada hizo muitikio miongoni mwa wazazi umekuwa duni jambo linalosababisha baadhi ya watoto kukosa chakula shuleni.

Dkt. Nkuba amesema kutokana na changamoto hiyo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kwa kushirikiana na TFNC wamekuja na mradi huu unaolenga kukuza uelewa wa masuala ya lishe.