TUNAKWENDA KUBORESHA UCHUMI WA KILA MWANARUFIJI- MCHENGERWA

Na Yohana Kidaga- Muhoro, Rufiji

Mgombea wa Ubunge Jimbo la Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kumchagua tena katika kipindi atahakikisha kwa pamoja wanafanya ujenzi wa uchumi kwa kila mwanarufiji wa jimbo hilo ili kuendelea kuboresha maisha yao.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kukiombea kura Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu kwa ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani katika kata ya Muhoro jimboni Rufiji jana Mhe. Mchengerwa amesema katika kuhakikisha miradi mingi ya maendeleo inakwenda kutekelezeka atakwenda kuiomba serikali kuweka kituo cha kupozea umeme ili kuwa na umeme wa uhakika ili kusaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kilimo ambayo tayari wawekezaji wameshajitokeza.

“Tayari tumepata wawekezaji wanaokwenda kujenga viwanda vikubwa hapa Rufiji, tarafa ya Muhoro, tumeshapata muwekezaji mkubwa ambaye anakwenda kuwekeza zaidi ya shilingi trioni 1.3 kwenye kiwanda kikubwa cha ndizi hali ambayo itatufanya kuuza ndizi duniani”. Amefafanua Mhe. Mchengerwa

Amesema akina mama zaidi ya 1000 na vijana zaidi ya 6000 wanakwena kujipatia ajira kwenye mradi huu ambapo amefafanua kuwa viwanda vitano vinakwenda kujengwa kwenye tarafa hiyo ya Muhoro na kuleta ajira nyingi kwa wananchi.
Ametoa wito kwa vijana na wananchi kujiandaa kimtizamo na kuwa tayari kufanya kazi kwa bidi ili wawekezaji hao waweze kuwaajiri badala ya kutegemea watu kutoka nje ya maeneo hayo.

Aidha amewashukuru kwa wananchi hao kuendelea kumchagua katika vipindi vyote kwa kura nyingi na kufafanua kuwa wamekuwa wakimchagua kwa kuwa wamejenga imani kubwa kuwa ni mtumishi wao ambaye siku zote amekuwa na ndoto za kuwaletea maendeleo ya kweli.


Leo, Mhe. Mchengerwa anaendelea na mikutano ya hadhara katika kata nyingine za Jimbo hilo kuomba kura kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa madiwani na kwake mwenyewe ili apewe ridhaa ya kuwaongoza tena katika kipindi hiki.

Mhe. Mchengerwa ni Mbunge wa tisa wa kuchaguliwa katika jimbo hilo la Rufiji toka lianzishwe na kuongozwa na wabunge kadhaa kuanzia mwanasiasa mkongwe nchini hayati Bibi Titi Mohamed ambapo anaelezewa kuwa ni miongoni mwa wabunge walioliletea maendeleo makubwa Jimbo hilo ukilinganisha na wabunge waliotangulia.

Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyoletwa na Mhe. Mchengerwa katika kipindi chake ni pamoja na ongezeko kubwa la Shule za Msingi na Sekondari, zahanati, vituo vya afya na Hospitali, ujenzi wa madaraja, barabara, huduma za maji na kuvutia wawekezaji katika jimbo hilo.