Dar es Salaam. Wadau wa Maendeleo Tanzania wamefanya mkutano wa pamoja kujadili juu ya mabadiliko ya mazingira ya ufadhili na uwekezaji katika miradi ya maendeleo na hatua zinazohitajika kufanikisha utekelezaji Dira ya Maendeleo 2050.
Majadiliano hayo yanafanyika wakati ambao Tanzania na mataifa mengine wanakabiliwa na upungufu wa fedha za misaada ambazo awali zilikuwa zikitumika kutekeleza miradi na afua mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na Marekani kabla ya Rais Donald Trump kuingia madarakani.
Waliyasema hayo katika mjadala ulioandaliwa Mfuko wa Mitaji ya Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) ukiwakutanisha viongozi wa serikali, mashirika ya kimataifa, balozi, sekta binafsi na asasi za kiraia, kwa lengo la kujadili njia za kutafsiri malengo ya kitaifa kuwa matokeo halisi kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa majadiliano hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda amesema upo umuhimu wa ushirikiano katika kukabiliana na mabadiliko ya ufadhili wa maendeleo.
“Huu ni wakati wa kuchukua hatua kwa pamoja na kuendana na Dira ya maendeleo ya Tanzania ya 2050. Kupitia mifumo mipya ya ufadhili wa maendeleo kama vile matumizi ya rasilimali za ndani, ushirikishwaji wa sekta binafsi, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, na matumizi ya hati fungani za kijani na za manispaa, tunaweza kuleta maendeleo jumuishi na yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi,” amesema Kaganda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa, Dk Fred Msemwa amesema ili kukabiliana na mabadiliko hayo Dira ya Maendeleo 2050 inalenga kuiweka sekta binafsi kama injini ya uchumi.
“Hili litafanyika huku serikali ikichukua hatua mbalimbali za kuwezesha na kupunguza hatari kwa wawekezaji,” amesema.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Susan Nyamondo amesema maarifa yaliyopatikana katika mkutano huo yatasaidia kuoanisha vipaumbele vya serikali na mikakati ya washirika wa maendeleo.
Alitolea mfano wa hati fungani ya kijani ya Tanga UWASA kama mfano wa jinsi ubunifu katika miradi ya maendeleo unavyoweza kusaidia kufanikisha malengo ya nchi.
Mkutano ulihusisha pia mjadala ambapo kati ya wana jopo alikuwepo, John Viner kutoka Ubalozi wa Sweden alieleza kuwa mwelekeo mpya wa misaada ya maendeleo wa Sweden unalenga kusimamia zaidi matumizi bora ya rasilimali na matumizi ya dhamana ili kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi.

Mkurugenzi wa Gatsby Africa-Shirika linalojihusisha na kutengeza ajira na ukuaji wa Uchumi, Samwel Kilua amesema washirika wa maendeleo wanapaswa kuzingatia mazingira halisi ya Tanzania na kuongeza thamani kwenye miradi iliyopo badala ya kufanya kazi kwa kujitenga.
Mkutano huo pia uliangazia mafanikio ya miradi ya UNCDF nchini Tanzania, ikiwemo miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi, kusaidia biashara ndogo na za kati kifedha kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, na uwekezaji katika mifumo ya chakula ya kilimo.
Pia ulionyesha mifumo kiubunifu ya ufadhili kama hati fungani za kijani, uwekezaji unaozingatia viwango.