WAKIMBIZA MWENGE WAANDAMIZI WATUNUKIWA KWA MARA YA KWANZA -RIDHIWANI KIKWETE ATOA HESHIMA YA KIPEKEE

Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, imetambua rasmi mchango wa waliowahi kuwa viongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa kuwatuza hati za shukrani, ikiwa ni heshima kwa uzalendo wao uliotukuka.Akizungumza katika kilele cha mbio hizo zilizohitimishwa kitaifa Oktoba 14, 2025 katika Viwanja vya Sokoine jijini Mbeya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, alisema kuwa tukio hilo ni hatua ya kihistoria na heshima kwa wazee hao waliolitumikia taifa kwa moyo wa kizalendo.

Miongoni mwa waliotunukiwa hati za shukrani na mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ni pamoja na Balozi Christopher Liundi (85) ,Meja Jenerali Mstaafu Zawadi Madawili (76) ,Mwanamke wa kwanza kuwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka 1975 akiwa na cheo cha Luteni, Jordan Rugimbana (59) Julius Tweneshe (62) na Meja Musa Ng’omambo
Kwa mujibu wa Ridhiwani Kikwete, tangu kuanzishwa kwa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 1964, jumla ya vijana 339 wamepata heshima ya kuukimbiza Mwenge katika kipindi cha miaka 61, wakiwa mstari wa mbele katika kueneza ujumbe wa mshikamano, amani na maendeleo.
Katika hafla hiyo, Mkoa wa Pwani umetunukiwa cheti na kikombe maalumu kwa kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025. 
Aidha, Halmashauri ya Chalinze iliibuka mshindi wa kwanza wa mbio hizo katika Kanda ya Nne, inayojumuisha mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara, Kigoma, Katavi na Rukwa.
Sherehe hizo pia zilipambwa na burudani mbalimbali, kauli mbiu za kitaifa, na tafakari juu ya mchango wa vijana katika kulijenga taifa kupitia dhana ya Mwenge wa Uhuru.