Wakulima wapewa mbinu kuimarisha zao la kahawa

Songwe. Katika kuhakikisha kuwa zao la kahawa aina ya Arabika kutoka Nyanda za juu Kusini linaendelea kufanya vizuri kwenye soko la kimataifa, wakulima wa kahawa wilayani Mbozi mkoani Songwe, wameanza kupewa  mafunzo ya kitaalamu pamoja na miche ya miti ya matunda na kivuli.

Hatua hiyo inalenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha ustahimilivu wa zao hilo.

Mafunzo hayo yametolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Solidaridad kwa kushirikiana na Serikali , ambapo wakulima wamefundishwa mbinu za kilimo mseto za kuchanganya zao la kahawa na mazao mengine rafiki kwa mazingira.

Wananchi wakipewa elimu ya upandaji miti kuchanganya na zao kwa lengo la kutunza mazingira na kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa nyanda za juu kusini Tanzania .Picha na Denis Sinkonde

Msimamizi wa mradi huo kutoka Solidaridad, Roselaida Ngowi amesema unalenga kuboresha uzalishaji wa zao la kahawa ambapo jitihada hizo zitasaidia kuboresha uzalishaji au kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao hilo, kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo au mbinu bora za kilimo cha kahawa kwa wakulima.

“Baada ya wakulima kupata mafunzo haya yatawasaidia kuelimisha jamii kwa ujumla kwani mradi huu pia unasaidia kuzalisha miti ya kivuli, mafunzo haya yamewasaidia wakulima kupata elimu ya sahihi ya kupangilia miti ya kivuli katika mashamba ya kahawa na kupata tija,” amesema Ngowi.

Amesema mafunzo hayo yatawasaidia wakulima kurutubisha udongo, kurekebisha hali ya hewa ili kuleta ustahimilivu wa mazingira na kiuchumi katika sekta ya zao la kahawa kwa wakulima ndani ya mikoa ya Songwe na Mbeya na Taifa kwa ujumla.

Meneja wa Kituo cha Utafiti wa Kahawa (TACRI) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dismas Pangalas amesema mafunzo hayo yamejikita kubainisha, kupendekeza na kutoa mwongozo wa aina ya miti inayofaa kuchanganya kwenye mashamba ya kahawa.

Mmoja wa wakulima wa zao la kahawa wilayani Mbozi akiwa kwenye kichanja Cha kuanikia zao la kahawa.picha na Denis Sinkonde

Amesema hatua hiyo  itasaidia  kwa kupata kivuli kitakachowezesha kukabilia na hali ya jua kali na ukame, hivyo wakulima wamepata fursa kujua mpangilio sahihi unaofaa katika kupanda kahawa, sambamba na miti ya kivuli.

Mkuu wa Divisheni ya Mifugo, Uvuvi na kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Nipwapwacha, amewapongeza wakulima kwa ushiriki wao na kuwasihi kutumia vyema elimu waliyopewa ili kuboresha maisha yao na kuongeza ushindani wa uzalishaji wa zao la kahawa ya Tanzania duniani.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine, mkufunzi Maria Mwazembe amesema kupitia kilimo mseto amejifunza kuwa kuchanganya kilimo cha kahawa na miti ya kivuli pamoja na miti matunda kama maparachichi na ndizi kunaweza kukupunguzia gharama ya kusimamia shamba.