Watu Wanne Wakamatwa Dar kwa Kumiliki Vyombo vya Habari Bila Leseni – Video – Global Publishers



Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewatia mbaroni watu wanne kwa tuhuma za kumiliki na kuendesha vyombo vya habari bila leseni halali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema waliokamatwa ni Japhet Alex, Joseph Mabe, Tegemeo Zacharia, na Eliah Pius.

Kamanda Muliro amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakitoa taarifa na kusambaza maudhui mtandaoni bila kuwa na vibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Idara ya Habari – MAELEZO, kinyume na sheria za nchi.

Ameongeza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao mara baada ya upelelezi kukamilika, huku akitoa onyo kwa watu wote wanaojihusisha na shughuli za utangazaji, uandishi au usambazaji wa habari bila kufuata taratibu za kisheria.

“Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaoendesha shughuli za habari bila vibali. Tunawataka wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanakuwa na leseni zinazotambulika kisheria,” amesema Kamanda Muliro.