Watuhumiwa 17 Mbaroni Kwa Wizi Wa Pikipiki Zanzibar – Global Publishers



Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja linawashikilia watuhumiwa 17 waliohusika katika makosa ya wizi wa pikipiki ambazo ziliibiwa na kuuzwa maeneo mbalimbali ndani ya Zanzibar.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishma Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu amesema kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kushirikiana na mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja lilifanya operesheni yenye lengo la kutokomeza wizi wa vyombo vya moto hususani Pikipiki.

Kamanda Mchomvu amebainisha kwamba, Katika operesheni hiyo limefanikiwa kuokoa jumla ya pikipiki 23 na kuwakamata watuhumiwa 17 wanaojihusisha na vitendo vya wizi, upokeaji wa mali za wizi pamoja na uuzaji wa mali za wizi.

Hivyo, amewaomba wananchi waliopatwa na kadhia ya kuibiwa vyombo vya moto wafike kituo cha Polisi Bububu kwa ajili ya kutambua vyombo hivyo na kupewa utaratibu utakaowawezesha kukabidhiwa mali zao.

Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shilla, amesema Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi na kuhakikisha kwamba katika kipindi hiki cha mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025 hakuna vitendo vinavyoweza kuleta uvunjifu wa amani.

Aidha, amewapongeza wananchi kwa kuendelea kushiriki kwenye shughuli za kampeni kistarabu jambo ambalo linadumisha amani na kufanyika kwa shughuli hizo kwa usalama.

Hata hivyo, amewahakikishia waandishi wa habari kwamba, Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana nao kwani linatambua kuwa, vyombo vya habari ni miongoni mwa wadau muhimu katika kufikisha ujumbe kwa wananchi.