Airtel Money Tanzania yafanya mazungumzo ya kimkakati na COPRA kuimarisha ujumuishi wa kifedha katika sekta ya kilimo

Dar es Salaam, Tanzania, Airtel Money Tanzania imefanya mazungumzo ya kimkakati na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), yenye lengo la kuimarisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali katika sekta ya kilimo. Mazungumzo hayo yanachochea fursa za ushirikiano zitakazowezesha kuimarisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali katika sekta ya kilimo nchini.

Mazungumzo hayo yanalenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kifedha katika kilimo biashara, hasa katika uwezeshaji wa wakulima na wadau wa sekta hii kufanya malipo, kuweka akiba na kupata huduma muhimu za kifedha kupitia majukwaa ya kidijitali kama Airtel Money.

Hatua hii ni sehemu ya juhudi endelevu za kukuza ujumuishi wa kifedha, kuongeza ufanisi katika minyororo ya thamani na kuimarisha ushiriki wa wakulima katika mifumo rasmi ya uchumi.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Andrew Rugambo, amesema: “Airtel Money inaamini kuwa teknolojia ya kifedha ni chachu ya mabadiliko katika sekta ya kilimo.

Kupitia ushirikiano huo na COPRA, tunalenga kuwawezesha wakulima kupata huduma bora za kifedha kwa urahisi zaidi, kuongeza uwazi katika malipo na kukuza uchumi wa wakulima kupitia mifumo ya kidijitali.” Amesema Bw. Rugambo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Madeje Mlola, amesema hatua hiyo muhimu itarahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima na wadau wetu.

Ushirikiano huu utasaidia kuongeza ufanisi katika minyororo ya thamani ya mazao, kurahisisha malipo, kuhakikisha usalama wa fedha za wakulima na kuimarisha ushiriki wa wakulima katika mifumo rasmi ya kifedha.” Amesema Mkurugenzi Mkuu Mlola.