Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori amesema benki hiyo imejipanga kikamilifu kuwa mshirika wa wawekezaji wanaotaka kuchangamkia fursa za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Uwekezaji huo utakuwa hususani nchini Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako benki hiyo inaendesha shughuli zake.
Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 kando ya Mkutano wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) jijini Washington, Profesa Mori amesema dira ya CRDB ni kuwa daraja kati ya mitaji ya kimataifa na masoko yanayokua kwa kasi barani Afrika.
“Benki hii inaona fursa kubwa katika sekta za madini, utalii, viwanda na kilimo, ambazo ni injini kuu za ukuaji wa uchumi wa kanda,” amesema Profesa Mori.
Amesema CRDB imejipanga kuwa mwezeshaji wa uwekezaji katika sekta hizo muhimu, kwa kutumia uwezo wake wa kifedha, mtandao wa kikanda na mifumo imara ya kifedha inayowaamini wawekezaji.
Profesa Mori amesema CRDB, yenye mizania ya takribani shilingi 20 trilioni, inaonyesha uimara wa mtaji na ukwasi wa kutosha, hali inayoiweka kuwa benki inayoaminika zaidi Afrika Mashariki.
Amesema benki hiyo inawaalika wawekezaji kutoka kote duniani kuangalia upya fursa zilizopo Afrika Mashariki.
“Ukanda huu una utajiri wa rasilimali, nguvu kazi changa na miundombinu inayoimarika, jambo linaloufanya kuwa eneo lenye matumaini makubwa ya uwekezaji wa muda mrefu.”
“Benki ya CRDB iko tayari, ikiwa na nguvu ya kifedha, utaalamu wa kikanda na uhusiano wa kimataifa kufanya kazi bega kwa bega na wawekezaji wanaotaka kuwa sehemu ya safari ya ukuaji wa Afrika,” amesema.
Amesema kwa sasa, Benki ya CRDB inahudumia wateja zaidi ya milioni 4 kwa Tanzania, Burundi na DRC, ikiwa na matawi zaidi ya 260, mawakala 25,000 na ATM 600, huku zaidi ya asilimia 90 ya miamala ikifanyika kupitia SimBanking na Internet Banking.
Pia, amesema upanuzi wa benki hiyo nchini Burundi na DRC umeunda jukwaa thabiti la kuwezesha biashara na uwekezaji wa kuvuka mipaka katika ukanda huo.
Profesa Mori amezungumzia kuhusu mageuzi ya kiteknolojia, ambayo wamewekeza kwa kiwango kikubwa kwa kuwahudumia wateja wao kwa urahisi na usalama zaidi.
“Tumewekeza kwa kiwango kikubwa katika teknolojia ya kisasa kuhakikisha tunawahudumia wateja wetu kwa urahisi na usalama zaidi. Uboreshaji wa mfumo mkuu wa benki na mifumo ya kadi kwa viwango vya kimataifa ni msingi unaotuwezesha kutoa huduma bora, salama na zenye ufanisi kwa wawekezaji.”
Aidha, Profesa Mori amesema CRDB inashiriki katika kusaidia mnyororo mzima wa thamani katika sekta za kilimo, viwanda na madini, kwa kuwaunganisha wawekezaji wakubwa na biashara ndogo na za kati.
Amesema: “Hii inahakikisha jamii zinanufaika kupitia ajira, minyororo ya usambazaji na ukuaji shirikishi.”
Kuhusu kibali cha Dubai, amesema hatua ya benki hiyo kupata kibali kutoka Mamlaka ya Huduma za Kifedha ya Dubai (DFSA) kufungua ofisi ya uwakilishi katika Kituo cha Kifedha cha Kimataifa cha Dubai (DIFC) ni muhimu.
“Dubai ni kitovu cha uwekezaji duniani. Uwepo wetu pale unaongeza uwezo wa kuwafikia wawekezaji na washirika wa maendeleo.”