……………………..
📍 Utafiti wa kina unaendelea katika Kitalu cha Lindi–Mtwara
📍 Dkt. Mataragio akagua maendeleo ya mradi, aagiza ukamilike kwa wakati
📍 Akagua pia mradi wa kuongeza uzalishaji wa gesi katika kitalu cha Mnazi Bay
📍 RC Mtwara asema Gesi Asilia ni kichocheo cha wawekezaji
📍 Mwenyekiti Kijiji cha Mwanamawa ataja faida za mradi kwa jamii ikiwemo ajira na miundombinu
Utafiti unaoendelea kufanyika katika Kitalu cha Lindi–Mtwara, mkoani Mtwara umeonesha dalili za uwepo wa Gesi Asilia, hususani katika vijiji vya Mnyundo na Mpapura, ambapo visima vya maji vilibainika kuvujisha gesi asilia.
Utafiti huo unajumuisha jumla ya vijiji 48 katika eneo la takriban kilomita za mraba 736 ambapo vijiji 40 vinatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (Mtwara DC) na vijiji 8 ni kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mtama (Mtama DC).
Katika ziara yake ya kukagua miradi ya gesi na mafuta mkoani Mtwara, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, amesema kuwa utafiti wa awali unaonesha uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa gesi asilia katika eneo hilo.
“Kwa kutumia data za mitetemo zilizokusanywa awali, tumebaini kwamba kuna hadi asilimia 32 ya uwezekano wa gesi kuwepo katika kitalu hiki,” amesema Dkt. Mataragio.
Ameeleza kuwa mahitaji ya gesi yamekuwa yakiongezeka katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, matumizi ya majumbani na usafirishaji – jambo linaloifanya Serikali kuendelea kuchochea utafutaji na uendelezaji wa vyanzo vya nishati hiyo ili kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mataragio pia alitembelea mradi wa kuongeza uzalishaji wa gesi katika eneo la Mnazi Bay, ambapo amebaini kuwa mradi huo uko katika hatua ya maandalizi kwa asilimia 68.
Mradi wa Mnazi Bay unahusisha visima vitatu vya gesi asilia, ambapo serikali inatarajia kuongeza uzalishaji kwa wastani wa futi za ujazo milioni 45 kwa siku kutoka kwenye visima viwili, huku kisima kimoja kikiwa ni kwa ajili ya utafiti zaidi wa uwepo wa gesi katika eneo lingine katika kitalu.
Dkt. Mataragio ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilishwa kwa mujibu wa ratiba ilivyopangwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amesema kuwa gesi asilia imekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji mkoani humo, na kwamba uwepo wa miradi hiyo umechochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
“Kwetu sisi watu wa Mtwara, sekta ya nishati ni msingi wa maendeleo na usalama wetu. Nawapongeza TPDC na wadau wote kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya gesi asilia ambayo pia imetoa ajira kwa wakazi wetu,” amesema Kanali Sawala.
Mjiolojia Paschal Njiko, ambaye ni Mkurugenzi wa Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi kutoka TPDC, amesema Shirika hilo litaendelea kusimamia wakandarasi kwa karibu ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na ndani ya bajeti.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanamawa, Bw. Selemani Hassani, ameishukuru Serikali kupitia TPDC kwa kuleta mradi huo kijijini kwao, na kueleza kuwa tayari wananchi wameanza kunufaika kupitia fursa za ajira na maboresho ya miundombinu.
“Kupitia mradi huu, tumepata barabara ndogondogo za mitaa ambazo zinarahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi. Wananchi pia wamepata kazi mbalimbali ambazo zimewawezesha kuongeza kipato,” amesema Mwenyekiti huyo.
Hadi sasa, zaidi ya ajira 1,200 za muda mfupi zimetolewa kwa wanachi wa Mtwara kupitia mradi wa kuchukua taarifa za mitetemo katika kitalu cha Lindi-Mtwara.