Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya mpira wa kikapu ya kimataifa ya Road to Basketball Africa League (BAL), Dar City, wataanza campeni ya kuwania nafasi kufuzu hatua ya 16 dhidi ya Djabal Basket Iconi ya Comoro.
Mchezo huo umepangwa kuanza saa 1.00 usiku kwenye uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) Masaki kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu la Tanzania (TBF), Mwenze Kabinda.
Kabinda alisema kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na Dar City imejiandaa vyema kuwania nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora iliyopangwa kufanyika nchini Afrika Kusini kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Alisema kuwa kila siku kutakuwa na mechi moja ambapo mechi ya mwisho itakuwa imepangwa kufanyika Jumapili. Mbali ya Dar City na Djabal Basket Iconi ya Comoro, timu nyingine ni Namuwongo Blazers kutoka Uganda.
“Maandalizi yamekamilika na timu zote zimewasili kwa ajili ya mashindano hayo. Timu mbili za kwanza zitafuzu hatua ya 16 bora iliyopangwa kufanyika nchini Afrika Kusini.
Dar City wana nafasi kubwa ya kufanya vyema katika mashindano haya kutokana na kuwa na wachezaji wazoefu,” alisema Kabinda.
Baadhi ya wachezahu hao ni Omary Ndula, Ally Faraj, Emmanuel Manyonyi, Amin Mkosa, Haji Mbegu, Foitus Ngaiza, Jamal Salum, Robert Shilla, Mhagachi Marwa na Hasheem Thabeet.
Pia wapo wachezaji wa kigeni ambao ni Deng Deng (Sudan Kusini), Raphiel Putney (USA), Makhi Mitchell (USA), Nirse Zouzoua (Ivory Coast) na Soueyman Diabate (Ivory Coast).
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kwa jina la Mwana FA, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kuisapoti timu ya kikapu ya Dar City.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwana FA amesema amefurahishwa na hatua ya Tanzania kuwa wachezaji wa ndani na nje ya nchi kwani inaonyesha maendeleo ya michezo nchini na mchango mkubwa wa wachezaji hao katika kukuza sifa za Taifa kimataifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameipongeza timu hiyo kwa uwekezaji mkubwa walioufanya, ikiwemo usajili wa kocha na wachezaji wa kigeni wenye uzoefu wa kimataifa.
Kutokana na mchezo wa kikapu kutokuwa na mashabiki wengi nchini, Chalamila amewaita wananchi kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo katika mashindano hayo.