Dk Mwinyi anavyozisaka kura akiendelea kutoa ahadi

Unguja. Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, ameahidi kuboresha mazingira ya biashara kuvutia uwekezaji wa ndani na nje.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Darajani ikiwa ni sehemu ya kampeni zake za kukutana na makundi tofauti, amesema hatua hiyo inalenga kukuza uchumi wa wananchi kupitia sekta ya biashara pamoja na kuongeza mvuto wa utalii kwa visiwa vya Zanzibar.

“Tunataka kuona Zanzibar inaendelea kuvutia wageni kwani ikiboresha mazingira ya wafanyabiashara, si tu kuwasaidia wafanyabiashara shughuli zao kuwa bora zaidi, bali pia kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza haiba ya mji na kuifanya Zanzibar ipendwe zaidi na watalii,” amesema Dk Mwinyi.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi akiangalia bidhaa mbalimbali alipotembelea na kuzungumza na wafanyabiashara wa Darajani Souk ikiwa ni sehemu ya kampeni za chama hicho.

Amesema meridhika na hali ya ufanyaji biashara katika eneo Darajani Souk kwani awali eneo hilo halikuwa katika mazingira mazuri ya kufanyia biashara na lilikuwa eneo dogo ukilinganisha na mazingira ya sasa.

Kwa mujibu wa mgombea huyo, iwapo wakirejea madarakani, wataendelea kujenga katika maeneo hayo ili yaweze kupatikana maduka zaidi kwani bado kuna idadi kubwa ya wafanyabiashara wanaweka biashara zao pembeni kwenye kuta jambo ambalo halikubaliki.

“Tunataka maduka au sehemu rasmi za kufanyia biashara, hilo tutalitekeleza ili watu wote wapate maeneo ya mazuri ya kufanyia biashara na sio kufanya biashara chini,” amesema Dk Mwinyi.

Wakati ikiboresha mazingira ya Biashara, pia wataendelea kujenga maegesho ili wananchi wanaoingia mjini wasipate shida ya kuegesha magari yao.

“Kuna mradi mkubwa ambao unajengwa katika maeneo ya Malindi kuwa kituo kikubwa cha mabasi kitakachokuwa na maegesho ili kuona hali ya watu kuegesha gari zao kila mahali liondoke,” amesema.

Amesema ana matumaini makubwa katika kipindi kifupi kijacho kuna mradi wa BIG Z ambao utatengeneza maduka kutoka Kariakoo hadi Kisiwandui upande wa kulia na kushoto na katikati kwani barabara hiyo itaondolewa magari na itakuwa ya kutembea kwa miguu au magari madogo.

“Mambo ya Zanzibar yatakuwa makubwa kwani tuna Tax za majini na tutaendelea kuzisambaza na mabasi ya umeme yanakuja yapo njiani ili kituo hiki cha Malindi kiweze kubeba wananchi na gari zitakazoingia mji Mkongwe zitakuwa za umeme ili kupunguza athari ya majengo ya zamani na kudumisha urithi wa mji huo darajani itakuwa kama Ulaya,” amesema.

Akizungumzia barabara kutoka Mnazi Mmoja hadi Malindi, mgombea huyo amesema itajengwa upya na kuwa ya njia nne yenye maeneo ya watembea kwa miguu, sehemu ya baskeli lengo ni kulifanya eneo hilo kuwa la biashara zaidi.

Akizungumzia hali ya amani na utulivu nchini, mgombea urais huyo amesema hata kama asingefanikiwa katika utekelezaji wa maendeleo ya aina yoyote lakini amani iliyopo hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi watu kukaa vizuri hayo ni mafanikio makubwa.

“Watu katika kipindi hichi walikuwa na hofu hawatoki kufanya shughuli zao za kibiashara wapo nyumbani wanaogopa uchaguzi lakini sasa hivi mambo mazuri wanafanya biashara na nakwambieni hata siku ya Oktoba 29 nendeni kapigeni kura alafu ukimaliza njoo ufungue duka lako amani itakuwepo,” amesema.

Amewasisitiza wananchi wakitaka kuwa na amani ya kweli, wakichague Chama cha Mapinduzi kwa kuwa ndicho chama pekee kinachohuburi amani umoja na mshikamano.

Amewaomba kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili CCM ishinde kwa kishindo kwa asilimia 90 na kuondoa malalamiko kwani uzoefu unaonesha watu wengi hawaendi kupiga kura.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk Mohammed Said Mohammed amesema ndani ya miaka iliyopita walipita eneo hilo kuomba ridhaa kuongoza na Rais aliwaahidi kutengeneza mazingira bora kwa wafanyabiashara wote na jambo hilo amelitekeleza kwa vitendo.

Amesema CCM haikubahatisha kumteua kugombea nafasi hiyo kwani chama kilimuona  ana sifa ya kuiongoza Zanzibar kwani ni kiongozi mwadilifu anayetoa ahadi na kuitekeleza, kiongozi anaewapenda watu wake na ana utu wa kupitiliza.

Amesema mbali na sifa hizo pia mgombea huyo ni kiongozi imara, sio mbabaifu na mwenye kuhubiri amani, umoja na mshikamano ambao ndio msingi wa maendeleo.

Amewakumbusha wafanyabiashara na wananchi wakikichagua Chama cha Mapinduzi na wagombea wake ndio wamechagua maendeleo yao.

Awali, akisoma risala kwa niaba ya wafanyabiashara wa eneo hilo, Iptisam Mohamed Rashid kisoma risala kwa niaba ya wafanyabiashara wa Darajani, amesema eneo hilo hivi sasa lina wafanyabiashara wa maduka 540 ambapo hapo nyuma kulikuwa na kontena 44 sawa na ogezeko la maduka na wafanyabiashara 500.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi akiangalia bidhaa mbalimbali alipotembelea na kuzungumza na wafanyabiashara wa Darajani Souk ikiwa ni sehemu ya kampeni za chama hicho.

Amepongeza hatua ya kuwekewa kituo cha daladala karibu na maduka yao ili kuongeza idadi ya wateja katika maeneo yao ya biashara.

“Kutokana na faida hizo pamoja na mazingira mazuri, bustani, maegesho ya magari imechangia katika ongezeko la ajira hasa kwa vijana, upatikanaji wa mikopo isiyo na riba,” amesema.