DKT.SERERA:SERIKALI ITAENDELEA KUISAIDIA FCC KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UDHIBITI WA BIDHAA BANDIA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Serera,akizungumza  leo, Oktoba 16, 2025, wakati wa ziara ya pamoja kati ya Menejimenti ya FCC na Wizara ya Viwanda na Biashara katika Kituo cha Forodha cha Horohoro kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, muda mfupi baada ya kutembelea Bandari ya Tanga.

Na.Mwandishi Wetu

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Serera, amewapongeza watumishi wa Tume ya Ushindani (FCC) kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kudhibiti bidhaa bandia nchini.

Dkt. Serera ametoa pongezi hizo leo, Oktoba 16, 2025, wakati wa ziara ya pamoja kati ya Menejimenti ya FCC na Wizara ya Viwanda na Biashara katika Kituo cha Forodha cha Horohoro kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, muda mfupi baada ya kutembelea Bandari ya Tanga. Ziara hiyo ilikuwa ni sehemu ya hitimisho la semina ya siku mbili iliyolenga kuimarisha uelewa kuhusu masuala ya ushindani, ulinzi wa walaji na udhibiti wa bidhaa bandia.

Amesema kuwa Kituo cha Forodha cha Horohoro kinahudumia wananchi wa ndani na nje ya nchi, hivyo ni muhimu kwa watumishi wa FCC kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na umakini mkubwa.

Aidha, ameongeza kuwa serikali ina imani na weledi wa watumishi wa FCC, lakini akatahadharisha kuwa wachache wasiowaadilifu wanaweza kuharibu sifa na ubora wa huduma zinazotolewa.

“Kama Serikali, tupo kwa ajili ya kuchagiza jitihada kubwa mnazozifanya FCC. Kama kutakuwa na changamoto, tutazichukua na kuzifanyia kazi ili muendelee kuwalinda walaji,” amesema  Dkt. Serera.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema taasisi hiyo imejikita katika kudhibiti bidhaa bandia kuingia nchini kwa kuhakikisha bidhaa zinakuwa na alama sahihi zinazoonesha mahali zilitoka na uhalisia wake.

Aidha amebainisha kuwa FCC inaendelea na mikakati ya kufungua ofisi mikoani na kuanza kutumia mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ujulikanao kama Tanoga, unaohusisha taasisi za ukaguzi ambazo hazina mifumo yao ya ndani.

Awali, Meneja Msaidizi wa Forodha Mkoa wa Tanga, Bw. Joseph Raymond, amesema kuwa Kituo cha Forodha cha Horohoro kinafanya ukaguzi wa bidhaa zinazoingia na kutoka nje ya nchi kwa kushirikiana kwa karibu na vitengo vyote vilivyopo mpakani, jambo linaloonesha mazingira mazuri ya utendaji kazi wa pamoja.