Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu ya kikapu ya Dar City katika mashindano ya kimataifa yanayotarajiwa kuanza Oktoba 17, 2025 katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini Dar es Salaam.
Mwinjuma alisema amefurahishwa na hatua ya uongozi wa Dar City kuunda timu imara inayojumuisha wachezaji kutoka ndani na nje ya nchi, akibainisha kuwa hatua hiyo inaongeza chachu ya maendeleo ya michezo nchini.
“Nimefurahishwa kuona Dar City wameweka nguvu kubwa katika kuendeleza mchezo wa kikapu, na hasa kuona wachezaji wa kimataifa wakishirikiana na wazawa. Hii ni fursa ya kipekee kwa vijana wetu kujifunza,” alisema Mwinjuma.
Akimtaja mchezaji nyota wa Tanzania, Hashim Thabiti, Naibu Waziri huyo alisema mchango wake katika mchezo wa kikapu ni mkubwa na unaendelea kuhamasisha vijana wengi kufuata nyayo zake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliipongeza timu ya Dar City kwa uwekezaji walioufanya kupitia usajili wa kocha na wachezaji wa kigeni, akisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya dhati ya kuinua mchezo huo nchini.
Hata hivyo, Chalamila aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo, akisema: “Mpira wa kikapu bado hauna mashabiki wengi kama michezo mingine, hivyo ni muhimu Watanzania wakajitokeza kuunga mkono timu yetu.”
Mashindano hayo yanatarajiwa kuhusisha timu kutoka Uganda na Comoro, huku timu kutoka Burundi ikishindwa kushiriki kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao.
Naye mchezaji wa Dar City, Hashim Thabiti, alisema maandalizi yanaendelea vizuri na wamejiandaa kikamilifu kuipa ushindi Tanzania.
“Tupo tayari kutoa burudani na ushindi. Tunaomba Watanzania wajitokeze kutuunga mkono,” alisema Thabiti.
Mashindano hayo yatamalizika Oktoba 19, 2025, yakilenga kuimarisha ushirikiano wa michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.