Kasulu. Serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), wanatarajia kufuta hadhi ya ukimbizi kwa wakimbizi wa Burundi waishio katika kambi ya Nyarugusu na Nduta zilizopo mkoani Kigoma ifikapo Juni, 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo, Alhamisi Oktoba 16, 2025 na Mkurugenzi wa Idara ya Ukimbizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, Sudi Mwakibasi wakati akizungumza na wakimbizi kutoka Burundi katika kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu.
Baadhi ya wakimbizi kutoka nchini Burundi, wanaoishi katika kambi ya Nyarugusu, iliyopo wilayani Kasulu wakisikiliza maelezo yanatolewa na serikali kuhusu kufutiwa hadhi ya ukimbizi ifikapo Juni,2026 endapo hawatajiandikisha na kurejea nchini kwao kwa hiari
Amesema makubaliano hayo imefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa nchini Burundi kuna amani hivyo watatakiwa kuondoka ifikapo Juni 30, 2026.
Mwakibasi amesema wakimbizi hao kutoka Burundi wanahifadhiwa kwenye kambi za Nyarugusu wilaya ya Kasulu na Nduta Wilaya ya Kibondo hawana hadhi na sifa ya kuwa wakimbizi.

Mkurugenzi wa Idara ya Ukimbizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, Sudi Mwakibasi
Amesema wakimbizi hao kwa sasa wanapewa muda wa kujiandikisha kwa hiari na kurudishwa nchini kwao shughuli itakayofanyika hadi Juni, 2026 kisha itabandikwa orodha ya wakimbizi wanaotakiwa kuondoka, na watakaogoma watachukuliwa hatua kwa mujibu wa makubaliano ya pande tatu yaliyofanyika.
Mwakilishi Mkazi wa UNHCR, Barbara Bentum Dotse amesema kuwa asilimia 90 ya wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye makambi ya Nyarugusu na Nduta mkoani Kigoma hawana hadhi ya kuendelea kuwa wakimbizi na uamuzi pekee dhidi yao ni kurejea nchini mwao.
“Sababu kubwa ambayo imegundulika wakati wa mahojiano na wakimbizi hao inaonyesha kuwa wengi wana changamoto ya kutokuwa na mashamba, ajira na masuala ya kiuchumi mambo yanayoweza kushughulikiwa wakiwa nchini kwao na siyo kwenye kambi wakiishi kama wakimbizi,” amesema Dotse.

Baadhi ya wakimbizi kutoka nchini Burundi, wanaoishi katika kambi ya Nyarugusu, iliyopo wilayani Kasulu wakisikiliza maelezo yanatolewa na serikali kuhusu kufutiwa hadhi ya ukimbizi ifikapo Juni,2026 endapo hawatajiandikisha na kurejea nchini kwao kwa hiari
Balozi Mdogo wa Burundi katika ubalozi wa Kigoma Tanzania, Kekenwa Jeremia amesema kuwa amekuwa akishughulikia changamoto mbalimbali za wakimbizi hao lakini hakuna inayowafanya waendelee kuwa wakimbizi na nyumbani kwao nchini Burundi amani ipo ya kutosha hivyo, wakimbizi hao wanapaswa kurejea nchini mwao.
Mkuu wa Mkoa Kigoma, Simon Sirro amesema Serikali za Tanzania na Burundi zimekuwa na mahusiano mazuri ya kindugu na wananchi wa nchi hizo mbili wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali pamoja, hivyo wakimbizi hao kuendelea kuwa kambini kunawaondolea fursa ya kushiriki shughuli za kiuchumi.
“Kulingana na maazimio na makubaliano ya pande tatu, Serikali ya Tanzania, Burundi na UNHCR tupo tayari kusimamia na kutekeleza makubaliano hayo na niwaombe ndugu zangu wakimbizi ni muda mzuri wa kurejea nchini kwenu sasa badala ya kusubiri nyakati ngumu za kurudi nyumbani kwa lazima,” amesema Sirro.

Baadhi ya wakimbizi kutoka nchini Burundi, wanaoishi katika kambi ya Nyarugusu, iliyopo wilayani Kasulu wakisikiliza maelezo yanatolewa na serikali kuhusu kufutiwa hadhi ya ukimbizi ifikapo Juni,2026 endapo hawatajiandikisha na kurejea nchini kwao kwa hiari
Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wakimbizi kutoka nchi ya Burundi waliopo kambi ya Nyarugusu, wamesema kutokana na makubaliano ya pande hizo tatu wao wapo tayari kujiandikisha na kurejea nchini kwao kabla ya Juni, 2026.
Juma Nyandwi amesema ni vizuri kurudi nyumbani na kufanya shughuli za kimaendeleo na kuwa huru kuliko ukiwa kambini unashindwa kufanya shughuli za kiuchumi kutokana na sheria kukubana.
“Tutatakiwa kurudi nyumbani ili kushirikiana na wenzetu kujenga nchi yetu maana huwezi kujenga nchi yako ukiwa ugenini,” amesema Butungani Solanje.