Kinachosubiriwa kuhusu hatima ya ‘kutekwa’ Polepole

Dar es Salaam. Hatima ya shauri la maombi kuhusu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, itajulikana Ijumaa ijayo, Oktoba 24, 2025, Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, itakapotoa uamuzi.

Mahakama imepanga kutoa uamuzi wa shauri la maombi ya amri ya kumfikisha mahakamani au kumwachia kwa dhamana (Habeas Corpus) Polepole, baada ya kukamilika kwa usikilizwaji wa hoja za pande zote kwa njia ya maandishi.

Shauri hilo la maombi namba 24514/2025, linalosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salma Maghimbi, lilifunguliwa na wakili Peter Kibatala kwa niaba ya Polepole Oktoba 7, 2025, chini ya hati ya dharura.

Wajibu maombi ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC).

Shauri hilo lilipangwa kusikilizwa leo, Oktoba 16, 2025, na lilianza kwa mdomo kabla ya mahakama kubadili utaratibu na kuamuru lisikilizwe kwa njia ya maandishi.

Awali, lilipoanza kusikilizwa, Kibatala aliomba mahakama izingatie ushahidi uliowasilishwa mahakamani kupitia viapo vyote viwili, chake na cha Godfrey Polepole, ambaye ni mdogo wa Humphrey, na kiapo cha ziada cha Godfrey.

Amefafanua mambo machache yaliyoelezwa katika viapo vya awali, kisha akaanza kufafanua taarifa zilizoko kwenye kiapo cha ziada, akieleza kuwa kwa mujibu wa taarifa alizozipata Godfrey, ndugu yake Humphrey alichukuliwa na askari polisi.

Amesema kuna ushahidi wa picha ambao tayari umewasilishwa mahakamani, zikionesha aina ya gari lililotumika kumchukua Polepole, rangi, namba za usajili, na kwamba sehemu nyingine inaonesha michirizi ya damu katika eneo la mlango wa nyuma.

Hata hivyo, wakati Kibatala akianza kufafanua kuhusu ushahidi wa picha hizo, jopo la mawakili wa wajibu maombi kupitia Wakili wa Serikali, Ayoub Sanga, walipinga ufafanuzi huo.

Amemtaka Kibatala atoe maelezo ya jumla tu kuhusu kiapo hicho, si kuchambua aya moja moja, akidai utaratibu huo utachukua muda mrefu.

Amedai na wao wana viapo tisa, akahoji itachukua siku ngapi kama na wao watachambua aya moja moja.

Kibatala amepinga hoja hiyo akieleza haina msingi wa kisheria, akisisitiza kuendelea na utaratibu huo.

Kutokana na mvutano huo, Jaji Maghimbi aliahirisha shauri hilo kwa muda na kuelekeza kukutana na mawakili wa pande zote chemba.

Baada ya majadiliano, waliporejea mahakamani, Kibatala akatoa hoja ya kutaka shauri liendelee kusikilizwa kwa njia ya maandishi kuanzia alipoishia, kwa kuzingatia udharura wa shauri hilo.

“Sisi tutakuwa tayari kuwasilisha hoja zetu leo hii kabla ya saa 6:00 usiku,” amesema Kibatala, akiomba wajibu maombi wapewe muda mfupi wa kuwasilisha hoja zao.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edith Mauya ameeleza hawana pingamizi, kwa kuwa wao ndio waliofungua shauri, na kama wameona utaratibu huo utaharakisha, wanaunga mkono.

Amesema watakuwa tayari kuwasilisha hoja ifikapo Jumatatu, Oktoba 20, 2025, huku Kibatala akieleza watawasilisha majibu ya ziada kama yatakuwapo Jumanne, Oktoba 21, 2025.

Jaji Maghimbi ameelekeza kila upande uwasilishe hoja zake kwa muda huo, kisha akapanga kutoa uamuzi Oktoba 24, 2025.

Kwa mujibu wa maombi hayo, Kibatala anaeleza Polepole aliripotiwa kutekwa na watu wanaodhaniwa kuwa maofisa wa Jeshi la Polisi waliovamia nyumbani kwake Ununio, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Oktoba 6, 2025.

Anadai mpaka sasa hajashtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika mahakama yoyote ya kisheria na kwamba inaaminika amewekwa kizuizini mahali kusikojulikana na wajibu maombi.

“Hivyo, haki zake za kikatiba zimekiukwa bila sababu za msingi. Ustawi wa mwombaji unahitaji uangalizi na uingiliaji wa haraka, ikiwemo kujua hali ya maisha yake,” amedai Kibatala katika hati ya maombi.

Anaiomba mahakama iwaelekeze wajibu maombi wamuachie huru mwombaji (Polepole) kwa dhamana au wamfikishe katika mahakama ya kisheria na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.

Katika kiapo kinachounga mkono maombi hayo, Kibatala anaeleza mwombaji (Polepole) ni raia wa Tanzania ambaye ameitumikia nchi yake katika nafasi mbalimbali za Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Cuba na kwingineko.

Pia anaeleza katikati ya mwaka huu, kwa hiari yake, alijiuzulu wadhifa wa ubalozi, akieleza sababu mbalimbali zikiwamo kutoridhika na namna mambo yanavyoendeshwa ndani ya Serikali na nchini Tanzania.

Kibatala anaeleza katika taarifa zake ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara, Polepole amekuwa akilalamika kuwa usalama wake uko hatarini kutokana na vitisho ambavyo amekuwa akivipokea kutoka kwa watu wasiojulikana kutokana na msimamo wake katika masuala mbalimbali.

“Haya yamethibitishwa kwa umma na kaka wa mwombaji (Polepole), Godfrey na Agustino Polepole, kama ilivyothibitishwa katika taarifa za vyombo vya habari vya ndani,” amesema Kibatala katika kiapo chake.

Anadai mjibu maombi wa tano (ZPC – Jumanne Muliro) amenukuliwa katika taarifa za vyombo vya habari akitoa taarifa za kupuuza tuhuma hizo nzito za utekwaji wake.

Amesisitiza kuwa mpaka wakati anaapa kiapo hicho, mwombaji Polepole hajulikani mahali alipo na hakuna hata mmoja kati ya wajibu maombi ambaye ametoa mrejesho wowote kuhusu alipo, hali yake ya ustawi, na hadhi yake ya kisheria, jambo linaloongeza kiwango cha wasiwasi nchini.

“Nina sababu za kuamini wajibu maombi, na hasa mjibu wa tano (ZPC), ana ufahamu na yuko na mamlaka ya kumshikilia mwombaji,” amedai.