Kocha Mbelgiji ateta na Folz, Pantev

KOCHA wa Chippa United, Luc Eymael amesema itakuwa ni aibu kwa Romain Folz na Dimitar Pantev kama Yanga na Simba zitashindwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Eymael, ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Yanga, alisema kutokana na ubora wa vikosi vilivyoundwa na klabu hizo mbili, hakuna sababu ya kushindwa kufuzu hatua ya makundi msimu huu.

“Nitasema wazi, itakuwa ni aibu kwa makocha wa Simba na Yanga kama timu zao zitabwagwa na klabu kama Nsingizini Hotspurs ya Eswatini au Silver Strikers ya Malawi,” amesema Eymael akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Afrika Kusini.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji, alieleza kuwa viwango vya soka la Tanzania vimepiga hatua kubwa katika miaka ya hivi karibuni, hasa kupitia uwekezaji uliofanywa na klabu hizo mbili kubwa nchini.

“Simba na Yanga sasa ni timu za kiwango cha juu Afrika. Zina wachezaji wa kimataifa, zinalipa vizuri. Ukishindwa kushinda dhidi ya timu kutoka Eswatini au Malawi, unapaswa kujiuliza maswali magumu,” ameongeza.

Oktoba 18, mwaka huu, Yanga itakabiliana na Silver Strikers kwenye Uwanja wa Bingu uliopo Malawi, huku Oktoba 19, 2025, Simba nayo itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Nsingizini Hotspurs kwenye Uwanja wa Samhlolo huko Eswatini.

Eymael amesema hana shaka na uwezo wa wachezaji wa klabu hizo, lakini ametoa tahadhari kwamba makocha wanapaswa kuepuka kujiamini kupita kiasi na kuandaa timu zao kwa nidhamu.

“Nimewahi kuona makocha wanapoteza mechi rahisi kwa sababu ya kiburi au kujiamini. Katika michuano ya Afrika, kila dakika ni muhimu. Huwezi kuchukulia poa mechi yoyote,” amesema.

Akizungumzia makocha husika, Eymael alisema Folz ni kocha mwenye falsafa nzuri ya pasi fupi, lakini anapaswa kuhakikisha timu yake inakuwa na uhai mkubwa wa kushambulia. Kwa upande wa Pantev, alisema anatakiwa kuwa na hesabu kubwa tofauti na alipokuwa na Gaborone.

Kocha huyo alihitimisha kwa kusema kwamba anatarajia kuona timu hizo mbili zikitinga hatua ya makundi bila wasiwasi, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuthibitisha ukuaji wa soka la Tanzania kwenye ramani ya Afrika.

Mbali na Simba na Yanga ambazo zinaiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, Azam itakuwa na kibarua cha kukabiliana na KMKM huku Singida Black Stars ikiwa na mtihani wa kucheza dhidi ya Flambeau du Centre ya Burundi.