Kibaha. Wadau wakuu wa sheria serikalini wamejadiliana namna kufanya mageuzi ya kisasa katika mifumo ya kisheria inayosimamia uwekezaji katika taasisi za umma.
Wamebainisha namna sheria zilizopitwa na wakati na usimamizi dhaifu wa mikataba vinavyoweza kuhatarisha thamani ya uwekezaji wa umma unaokua kwa kasi.
Kwa sasa, thamani ya uwekezaji wa mashirika ya umma nchini imeongezeka na kufikia Sh92 trilioni ikilinganishwa na Sh86 trilioni mwaka uliopita.
Wakizungumza katika kikao kazi cha siku mbili kilichoanza leo Oktoba 16, 2025 kilichohusisha Ofisi ya Msajili wa Hazina, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, wadau hao wameshauri kufanyika maboresho ya sheria zinazoyaongoza mashirika ya umma, ambazo wamesema nyingi haziendani na kasi iliyopo.
Katika kikao kazi hicho kilichokuwa na kaulimbiu: “Nafasi ya taasisi kuu za kisheria za Serikali katika kulinda uwekezaji wa umma” suala la huduma kwa wateja katika taasisi za umma pia lilijadiliwa.
Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole ameeleza umuhimu wa kufanya maboresho ya sheria zinazoyaongoza mashirika ya umma, akionya mengi kati ya mashirika hayo yameanzishwa chini ya sheria ambazo haziendani tena na dira ya maendeleo ya sasa au ya baadaye ya Taifa.
“Taasisi nyingi ziliundwa miongo kadhaa iliyopita na bado zinaendeshwa kwa sheria za zamani ambazo hazina uhalisia na uchumi wa sasa wala matarajio ya miaka 20 hadi 25 ijayo,” amesema.
Njole amesisitiza kikao kazi hicho kuweka mikakati mahususi kuhakikisha taasisi hizo zinajengwa juu ya misingi imara ya kisheria.
Amesema mfumo wa kisheria wa Tanzania unapaswa kuendana na kasi ya uwekezaji wa umma na mageuzi ya utawala bora wa kampuni.
“Huenda mfumo wetu wa sasa wa kisheria haujaendana na kasi ya mashirika ya umma, Msajili wa Hazina (Nehemiah Mchechu) ameeleza maeneo ya changamoto, hatuna budi kuzitafutia suluhisho,” amesema.
Amesema kikao kazi hicho ni fursa muhimu kuoanisha mikakati ya Serikali kuhusu mwelekeo wa uwekezaji wa umma.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Posi, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya kisasa ya usimamizi wa mikataba ili kuzuia migogoro ya kisheria na kulinda mali za Serikali.
“Sehemu kubwa ya kesi za Serikali zinahusiana na mashirika ya umma. Hii inamaanisha tunapaswa kuimarisha uwezo wa kitaalamu na kuhakikisha mikataba inasimamiwa kwa kutumia zana za kisasa na utaalamu wa hali ya juu ili kupunguza hatari na hasara,” amesema.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, ameonya kuhusu usimamizi hafifu wa mikataba, akisema unaweza kuchelewesha au hata kuhujumu utekelezaji wa miradi ya Serikali.
“Ikiwa usimamizi wa mikataba utakuwa dhaifu, malengo ya Serikali yatachelewa au kushindwa kabisa kutekelezwa, hii itasababisha hata migogoro isiyo ya lazima,” amesema.
Amezungumzia mikataba inayosainiwa katika kila mwaka wa fedha, akisema ni kati ya 15,000 na 20,000, hivyo ufuatiliaji wake unahitaji usaidizi wa teknolojia.
“Tunaweka msisitizo zaidi katika kutumia mifumo ya kidijitali kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mikataba,” amesema.
Msajili wa Hazina, Mchechu, amesema Tanzania kwa sasa inasimamia zaidi ya taasisi za umma 300, ambayo ni ishara ya kupanuka kwa wigo wa mashirika ya umma katika sekta muhimu kama nishati, usafirishaji na fedha.
Amesema mapato ya Sh1.028 trilioni yaliyokusanywa mwaka huu kupitia gawio na michango kutoka taasisi za umma yanaonyesha kuimarika kwa utawala bora na usimamizi wa utendaji.
Mchechu amebainisha changamoto zilizopo katika kuongeza mchango wa taasisi za umma kwenye uchumi na kupunguza utegemezi kwa fedha za Serikali akieleza:
“Tumeanzisha KPIs (viashiria maalumu vya utendaji) kwa kila sekta ili kufuatilia na kusaidia utendaji wa taasisi hizo. Lengo letu ni taasisi ziweze kujitegemea.”
Amesema hatua hiyo inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inayolenga uimara wa kifedha.
Amesema wana lengo la kukusanya Sh2 trilioni kupitia gawio kufikia mwaka 2026, wakitumia teknolojia na mageuzi ya kisheria kuendeleza kasi hiyo.
Wadau katika kikao hicho wamekubaliana kuwapo ushirikiano thabiti kati ya taasisi za kisheria na zile za kifedha ili kulinda mali za umma na kuongeza tija ya uwekezaji kwenye taasisi hizo.