Mahakama yakataa kuhojiwa waliotoa viapo kesi ya Polepole

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeyakataa maombi ya mawakili wa wajibu maombi katika shauri la kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kuwaita kizimbani na kuwahoji watu waliokula viapo vilivyoambatanishwa katika hati ya maombi ya shauri hilo, akiwamo wakili wake, Peter Kibatala.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani jana Jumatano, Oktoba 15, 2025 na jopo la mawakili wa wajibu maombi katika shauri hilo, linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraji Nguka, wakati lilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Maombi hayo yalipingwa na jopo la mawakili wa mwombaji, linaloongozwa na Kibatala, wakidai yanalenga kuchelewesha usikilizwaji wa shauri hilo.

Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salma Maghimbi, anayesikiliza shauri hilo katika uamuzi alioutoa leo Alhamisi Oktoba 16, 2025, ameyakataa maombi hayo.

Katika uamuzi huo Jaji Maghimbi amesema anakubaliana na Kibatala kuwa shauri la kina Mdee lililorejewa mawakili wa wajibu maombi ni tofauti na lililopo mbele yake.

Amesema madai ya kukinzana kwa taarifa yaliyotolewa na mawakili wa wajibu maombi yataamriwa na mahakama, akieleza mawakili watakuwa na nafasi ya kuzieleza na si kuita mashahidi kwa ajili ya kuwahoji.

“Kwa mazingira ya shauri hili sioni sababu za msingi za kuita mashahidi kwa ajili ya mahojiano. Hivyo, maombi ya upande wa wajibu maombi yanakataliwa na shauri linaendelea kusikilizwa,” amesema.

Baada ya uamuzi huo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edith Mauya ameieleza mahakama kuwa waliwasilisha taarifa ya pingamizi la awali, lakini wameamua kuliondoa ili kuendelea na usikilizwaji wa shauri.

Kibatala ameridhia uamuzi wa wajibu maombi kuondoa pingamizi hilo na Mahakama ikatoa uamuzi wa kuliondoa.

Polepole anadaiwa kutekwa usiku wa Oktoba 6, 2025 na watu wasiojulikana waliovamia makazi yake eneo la Ununio, Dar es Salaam.

Oktoba 7, 2025, mawakili wake wakiongozwa na Kibatala walifungua shauri la maombi ya amri ya kumfikisha mahakamani au kumwachia kwa dhamana (Habeas corpus), chini ya hati ya dharura.

Wajibu maombi kwa mfuatano ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC).

Pamoja na mambo mengine, Kibatala katika kiapo chake kinachounga mkono maombi hayo anadai kuna sababu za kuamini kuwa wajibu maombi na hasa wa tano (ZPC) anaufahamu na ana mamlaka ya kumshikilia mwombaji.

Shauri hilo la maombi namba 24514/2025 lilipangwa kusikilizwa jana Oktoba 15 kwa kuhusisha pande zote, lakini kabla ya kuanza usikilizwaji ndipo mawakili wa wajibu maombi wakawasilisha maombi hayo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraji Nguka, akirejea vifungu vya sheria na uamuzi wa Mahakama Kuu katika moja ya mashauri yake, amesema katika shauri hilo kuna viapo viwili, kimoja cha Peter Kibatala na cha pili cha Godfrey Polepole.

Alisema mahakama ina mamlaka hayo chini ya kifungu cha 109 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Marejeo ya Mwaka 2023. Pia, aliirejesha mahakama katika uamuzi wake katika shauri la Halima Mdee na wenzake dhidi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) la mwaka 2023.

“Hivyo naiomba mahakama yako ituitie shahidi Peter Kibatala na Godfrey Polepole kwa ajili ya cross examination (maswali ya dodoso)” aliomba.

Akijibu ombi hilo, Kibatala alirejea uamuzi wa mahakama hiyo kwenye shauri hilo katika ombi la kumuita Christina Polepole, dawa wa Humphrey kutoa ushahidi kwa mdomo. Mahakama ililikataa ombi hilo kutokana na uharaka wa shauri hilo.

Alisema kwa kuzingatia uamuzi huo, kuruhusu maombi ya Jamhuri ni kurudi kulekule ambako uamuzi umeshatolewa.

Akizingumzia kesi ya Halima Mdee, Kibatala alisema lilikuwa shauri la maombi ya mapitio ya mahakama tofauti na lililopo la maombi ya mtu anayeshikiliwa kizuizini kufikishwa mahakamani au kuachiwa kwa dhamana.

Vilevile, alisema katika shauri hilo baada ya mahakama kuridhia maombi ya kuwaita baadhi ya wajibu maombi kuhojiwa kuhusu taarifa walizotoa kwenye viapo vyao, mawakili wa waombaji pia wanaiomba mahakama iridhie baadhi ya wajibu maombi kifika mahakamani kuhojiwa.

Kibatala alidai katika kiapo chake kama kilivyo cha wakili Edith Mauya ambaye pia ameapa kwa niaba ya ofisi ya ZCO, wameweka bayana kuwa wamepata taarifa walizozitoa kutokana na majukumu na taaluma yao kama mawakili, kwa hiyo wana kinga.

Alidai kwa kuwa katika shauri la Polepole pia kuna Wakili wa Serikali, Edith Mauya ametoa kiapo pamoja na watu wengine, akiwamo Mkuu wa Upelelezi wa Kanda ya Dar es Salaam (ZCO) Mafwele, hivyo Jamhuri wakiruhusiwa itafungua milango kwa wao kuwaita Mauya na kina Mafwele kwa ajili ya kuwauliza maswali ya dodoso.

“Maana haiwezekani kutoa haki hiyo upande mmoja tu,” amesema.

Kuhusu kifungu cha 109 cha CPA alichokirejea wakili Nguka, alidai kinaipa mamlaka hayo ya kumuita shahidi kumhoji au kutoa ufafanuzi na si kwa wadaawa.

Wakili wa Serikali Sanga amesema mahakama haijafungwa na uamuzi ilioutoa punde, kwani mazingira ya uamuzi huo na maombi yao ni tofauti akifafanua kuwa katika maombi yao walitaka kuleta ushahidi, lakini wao ni mashahidi ambao viapo viko mahakamani.

Alisema wao hawana tatizo la kuhojiwa waliotoa viapo kwa upande wao.