MAPESSA INTERTRADE YAPAMBANIA UJENZI VIWANDA VYA UCHENJUAJI, KEMIKALI CHUNYA

Kampuni ya Uuzaji wa Vifaa na Kemikali za Uchenjuaji Madini Chunya, MAPESSA Intertrade Ltd imeiomba Serikali  kuendelea kuhamasisha wadau na Wawekezaji kuanzisha viwanda vya utengenezaji Vifaa vya uchenjuaji  na kemikali  zinazotumika  katika uzalishaji wa  madini ya dhahabu ili viweze kupatikana kwa bei nafuu na kwa urahisi zaidi kwa  wachimbaji wadogo.

Akizungumza  na Madini Diary hivi karibuni, Mhasibu wa kampuni hiyo Joyce Ndolela alisema kuwa kutokana na gharama za vifaa hivyo kubwa kubwa, hupelekea baadhi ya wachimbaji wadogo kushindwa kumudu gharama na kueleza kwamba, jambo hilo linasababishwa na kutokuwepo kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo nchini na kueleza kuwa hiyo ni fursa kwa wawekezaji.

‘’Kama bidhaa hizi zingekuwa zinatengenezwa hapa hapa nchini, zingekuwa zinapatikana kwa bei nafuu na hivyo ingekuwa ahueni kwa wachimbaji wadogo kwasababu kwa hivi sasa inabidi tuagize nje,’’ anasema Joyce.

Kampuni ya MAPESSA ni ya mchimbaji, inauza vifaa mbalimbali zikiwemo compressor na mashine za kuchenjua mawe ya madini ambazo zinaweza kutumiwa kwenye migodi midogo na mikubwa ‘’Hapa kwetu mteja anaweza kuwekeza kidogo kidogo pindi anapokamilisha malipo yote anakabidhiwa vifaa vyake,’’ anaeleza Joyce.

Joyce ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kutumia mashine za kisasa badala ya njia za asili kwani zinasaidia kuepusha ajali na kuongeza uzalishaji huku akitoa wito kwa wanawake kutokuogopa kuingia katika sekta ya madini kupitia fursa mbalimbali.

Akizungumzia mchango wa madini kwenye biashara hiyo alisema mmiliki wa biashara hiyo ni mchimbaji ambaye amewekeza katika uuzaji wa vifaa na kemikali akilenga kurahisisha shughuli za madini. ‘’mtaji wa kuanzisha biashara hii aliupata kupitia uchimbaji na hii imewezesha pia na sisi kupata ajira hapa,’’ anasema Joyce.

Mapessa Intertrade Ltd ilianzishwa rasmi  2023, Itumbi Chunya kama kituo kidogo hadi  mwezi Juni 2025 ambapo makao makuu yake yalianzishwa Chunya mjini ikilenga kuwasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kisasa kuendana na teknolojia za kisasa kupitia bidhaa zinazouzwa na kampuni hiyo.

Kwa mantiki hiyo, Mapessa Intertrade inatoa mfano hai wa namna shughuli za madini zinavyoweza kuchochea biashara nyingine zinazosaidia maendeleo na uchumi wa ndani. Ushiriki katika sekta ya madini hauishii kwenye uchimbaji pekee – watanzania na wawekezaji wanaweza kushiriki katika hatua mbalimbali kama vile uzalishaji wa vifaa, usambazaji wa kemikali, usafirishaji na hata huduma za kitaalamu.

Serikali tayari imeweka mazingira wezeshi, hivyo huu ni wakati muafaka kwa wadau mbalimbali kuchangamkia fursa hii pana ya mnyororo wa madini ili kukuza ajira na mapato ndani ya nchi.

Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri

Madini ni Ajira, Uchumi na Maendeleo