Kocha Msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi raia wa Malawi, amepiga mkwara mzito, kisha mwisho wa siku akasema: “Wananchi watafurahi.”
Mabedi ambaye alitambulishwa Oktoba 13, 2025 kuchukua nafasi ya Manu Rodriguez, ametoa kauli hiyo wakati ameambatana na kikosi cha Yanga kilichoifuata Silver Strikers.
Kikosi cha Yanga ambacho leo Oktoba 16, 2025 kimeelekea Malawi kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili ikiwa ni mkondo wa kwanza, inasaka kufuzu makundi ya michuano hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa Jumamosi Oktoba 18, 2025 kwenye Uwanja wa Bingu nchini Malawi kuanzia saa 10:00 jioni huku marudiano ikiwa jijini Dar es Salaam, Oktoba 25, 2026.
Mabedi ameliambia Mwananspoti kuwa katika kikosi cha Silver Strikers, kuna wachezaji anawafahamu, hivyo itakuwa faida kubwa kwa Yanga kufanya vizuri.

“Mechi hii ni muhimu sana, ninarudi nyumbani tunakwenda kucheza na Silver Strikers ambayo ni timu ya nyumbani, tunakwenda kufanya kile tunachoweza ili kufanya vizuri na kwenda hatua inayofuata,” alisema Mabedi ambaye kabla ya kutua Yanga, alikuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Malawi.
“Kucheza na timu yenye watu ambao unawafahamu vizuri ni faida kubwa sana kwetu Yanga, ninawajua baadhi ya wachezaji niliowafundisha timu ya taifa na kuna baadhi ya vijana chini ya miaka 20 wamepandishwa timu ya wakubwa, ninawafahamu vizuri sana lakini mwisho wa yote tunatakiwa kwenda na kucheza kwa kupambana kufanya vizuri.
“Silver Strikers ni timu nzuri, huwezi kuidharau, ndiyo maana nasema tunahitaji kuongeza juhudi ambazo zinaweza kutufanikisha tufikie malengo,” amesema kocha huyo mwenye leseni A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Akizungumzia uwepo wake ndani ya Yanga kwa siku kadhaa namna alivyowaona wachezaji wa timu hiyo, Mabedi amesema: “Wachezaji wa Yanga wanapambana sana mazoezini wakionyesha matumaini ya kuendelea mbele na kufanya vizuri zaidi, ninaamini mashabiki watafurahia.”
Yanga ambayo msimu huu haijapoteza mechi yoyote ya mashindano kati ya ilizocheza ikishinda nne na sare moja huku safu ya ulinzi ikizuia nyavu zisiguswe, inakutana na Silver Strikers ambayo mechi tatu zilizopita haijaonja ushindi zaidi ya sare mbili na kupoteza moja.
Hata hivyo, hilo halijamfanya Mabedi kuidharau Silver Strikers akisema: “Katika soka unaweza kuona timu inashindwa kupata matokeo mazuri, lakini inakuja kufanya vizuri dhidi ya timu kubwa. Yanga ni timu kubwa, hivyo mpinzani anayekuja lazima aongeze juhudi zaidi, kwa hiyo hatuchukulii faida ya wao kutofanya vizuri.”

Rekodi zinaonyesha Silver Strikers ilishawahi kukutana na Yanga katika Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup), ilikuwa mwaka 1986 jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda 3-1 ikiwa ni mechi ya Kundi A.
Silver Strikers imefuzu hatua ya pili baada ya kuitoa Elgeco Plus ya Madagascar kwa faida ya bao la ugenini kufuatia kutoka 1-1 ugenini, na 0-0 nyumbani.
Kwa upande wa Yanga, imeitoa Wiliete SC ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0. Ilianza ugenini kushinda 3-0, ikamalizia nyumbani ushindi mwingine wa mabao 2-0.
Katika kikosi cha Silver Strikers kinachofundishwa na Peter Mgangira, mastaa wanaotumika zaidi ni Uchizi Vunga na Levison Maganizo wanaocheza eneo la kiungo.
Wengine ni kipa George Chikooka, Maxwell Paipi, Dan Sandukira, McDonald Lameck, Nickson Mwase, Stanie Davie na Chinsisi Maonga, ambao ndio waliocheza mechi zote mbili dhidi ya Elgeco PLUS na kuitoa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.