Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la 15 la Afya ya Kinywa na Meno lililofanyika leo Oktoba 15, 2025 MUHAS, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzobo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la 15 la Afya ya Kinywa na Meno.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya (kushoto) akimkabidhi Zawadi mgeni rasmi wa Kongamano la 15 la Afya ya Kinywa na Meno Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe.
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimewakutanisha wataalamu wa afya ya kinywa na meno, watafiti, watunga sera na wadau mbalimbali kupitia Kongamano la 15 la Afya ya Kinywa na Meno lenye lengo kujadiliana na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno nchini.
Imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali imetumia shilingi bilioni 17 kununua mitambo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno katika hospitali zote nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo lililofanyika leo Oktoba 15, 2025 MUHAS, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesisisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kuelimishwa kuhusu afya ya kinywa na meno, huku akieleza kuwa meno ni kiungo muhimu kwa afya ya binadamu na huchangia kwa kiasi kikubwa katika mfumo wa umeng’enyaji wa chakula.
“Tunapaswa kuzingatia ushauri wa wataalamu ili kulinda afya ya kinywa na meno. Ushirikiano kati ya Serikali, taasisi na wananchi ni muhimu katika kufanikisha hili,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya, amesema kuwa kongamano hilo limehusisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa afya ya kinywa na meno, watafiti, na watunga sera, kwa lengo la kuibua mapendekezo yenye tija kwa maendeleo ya sekta hiyo.
“Mapendekezo yatakayotolewa yatawasilishwa kwa mamlaka husika kama Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais ili yafanyiwe kazi kwa haraka. Pia, tunapitia mitaala yetu ili kuhakikisha inakwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia, kwa kutumia vifaa vya kidijitali katika ufundishaji na utoaji wa huduma,” amesema Prof. Balandya.
Ameongeza kuwa MUHAS inazalisha wataalamu wa kinywa na meno kuanzia ngazi ya stashahada, shahada, hadi uzamivu, lakini bado kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu hao nchini.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzobo, ameeleza kuwa hali ya afya ya kinywa na meno nchini si ya kuridhisha, ambapo tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 76.5 ya watu wazima wanakabiliwa na tatizo la kuoza meno, kwa watoto, kiwango hicho kimefikia asilimia 31.1.
Aidha, asilimia 68 ya watu wazima na asilimia 57 ya watoto wana tatizo la ugonjwa wa fizi, huku asilimia 33.1 ya wananchi wakiwa na changamoto ya meno ya kuwahiya, hasa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mwanza, Tabora na Shinyanga. Zaidi ya hapo, asilimia 62 ya Watanzania wana mpangilio usio sahihi wa meno kwenye vinywa vyao.
Dkt. Nzobo amebainisha kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa wataalamu, ambapo nchi inahitaji madaktari bingwa wa kinywa na meno wapatao 300, lakini waliopo hawazidi 100.
Aidha, kuna uhitaji wa madaktari wa shahada ya kwanza 970, huku waliopo wakiwa ni 350 tu. Kwa upande wa matabibu wa meno, taifa linahitaji 2,600, lakini waliopo ni 700 pekee wanaotoa huduma katika vituo mbalimbali.