Dar es Salaam. Mwangwi wa wito wa amani kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu umeendelea kusikika masikioni mwa Watanzania, safari hii ukivuma kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Jeshi hilo limesema linaendelea kufuatilia kwa karibu na kutathmini hali ya ulinzi na usalama nchini kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 na 29, 2025, kama ilivyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
“Kwa ujumla, jeshi linaridhishwa na hali ya usalama iliyopo nchini katika kipindi hiki ambacho vyama vya siasa vinaendesha kampeni zao kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, kuheshimiana na kuvumiliana kunakooneshwa kupitia wagombea wa ngazi za urais, ubunge na udiwani,” imeeleza taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo, Oktoba 16, 2025, na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Bernard Mlunga.
Amesema jeshi linaviomba vyama vya siasa kuendeleza hali ya amani na utulivu wakati wote wa kampeni, siku ya kupiga kura na baada ya kupiga kura.
JWTZ pia limeipongeza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kwa jinsi vinavyoendelea kusimamia hali ya usalama katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Mlunga amesema jeshi linawapongeza wananchi kwa kuendelea kutumia haki yao ya msingi ya kushiriki kwa amani na utulivu katika kusikiliza sera za vyama mbalimbali kupitia mikutano ya hadhara inayoendelea kufanywa na vyama vinavyoshiriki uchaguzi kwa ngazi tofauti, ili kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
Mbali na hayo, JWTZ limeutaka umma wa Watanzania kupuuza machapisho au taarifa ambazo zimekuwa zikionekana kwenye mitandao ya kijamii zikilihusisha jeshi na masuala ya siasa.
Jeshi hilo limesisitiza kuwa taarifa zote zinazolihusu jeshi zitatolewa na makao makuu yake kwa utaratibu rasmi wa mawasiliano kati ya jeshi na umma.
“Pamoja na hali ya amani na utulivu iliyopo, bado kumekuwa na baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati kutoka ndani na nje ya nchi wakitumia mitandao ya kijamii kupotosha umma kwa kuweka maudhui yenye kuleta uchochezi kwa kulihusisha jeshi na siasa ili kutimiza azma yao ya uvunjifu wa amani,” limesema jeshi hilo.
JWTZ imeeleza kuwa, likiwa sehemu ya vyombo vya ulinzi na usalama vyenye dhamana ya ulinzi nchini, linawahakikishia Watanzania wote kuwa hali ya amani, usalama na utulivu katika kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi ipo shwari.
Kwa nyakati tofauti, wito wa amani umekuwa ukitolewa na viongozi wa Serikali, wa dini na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu.
Oktoba 15, 2025, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, mjini Karagwe, alisema watakaothubutu kuandamana Oktoba 29, watakutana na visiki, akisema vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoko chini ya wizara yake vinaendelea kufanya kazi kwa weledi.
“Wako timamu kwa kushirikiana na vyombo vingine kuhakikisha amani inaendelea kutamalaki. Hakutakuwa na mtu yeyote atakayethubutu kuandamana Oktoba 29, atakutana na visiki,” alisema.
Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, Oktoba 13, 2025, akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam, aliwataka Watanzania Oktoba 29 wajitokeze kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka.
“Nataka kuwahakikishia Watanzania, amani ipo, wasiwe na wasiwasi wowote. Serikali ipo makini, vyombo vyetu vyote vya dola vimejiandaa kama ambavyo imekuwa ikifanya hivyo kwenye chaguzi zote zilizopita kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwenye mazingira tulivu na yenye amani,” alisema.
Msigwa alisema hakuna mtu atakayefanya kitu chochote na waachane na maneno yanayotengenezwa kwenye mitandao kutishia watu na kuaminisha vitu ambavyo havitatokea.
Oktoba 10, 2025, akijibu swali la mwandishi wa habari wa East Africa Radio kuhusu hamasa ya maandamano ya Oktoba 29 inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, alisema jeshi hilo limejiandaa vizuri kuwalinda Watanzania walio wema.
Swali hilo Misime alilijibu kupitia kipindi cha Super Breakfast akiwataka Watanzania wema waugane na jeshi hilo kuwakabili wahusika.
“Tuungane kuwakabili hao watu kwa namna gani…? Kuwapa elimu, kuwaambia wanachokipanga, wanachohamasisha, wanavyoona kasoro ndogo wanatumia kuchonganisha Watanzania, waviache na tuwasiwakubali,” alisema.
Misime alisema wanaohamasisha maandamano hayo ni wahalifu, na mhalifu yeyote yule anayeshambulia mifumo ya kisheria, saa zote hushambulia vyombo vya ulinzi na usalama.
“Wanajua wakidhoofisha vyombo vya ulinzi na usalama, uhalifu wao wataufanya. Tuwaambie, Jeshi la Polisi halidhoofishwi kwa namna hiyo, tupo imara na tuna mafunzo ya kutosha,” alisema.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Richard Mbunda, amesema inaonekana kuna watu wana vinyongo kuhusu namna uchaguzi ulivyoratibiwa.
“Wanaona mamlaka yao kama wananchi ya kuchagua ni kama imeporwa, na siyo wao ndio wana mamlaka ya kuamua nani awaongoze,” amesema.
Amesema yapo baadhi ya matamko yanayotolewa na baadhi ya watu kwenye jamii yanachochea hasira za watu.
“Ninachotamani kuona ni Serikali kusaka maridhiano, kwa sababu kuna watu wengi wana manung’uniko. Wapo waliozuiwa kuabudu, wapo wagombea walioenguliwa, wapo ambao chama chao hakishiriki uchaguzi. Kipindi kama hiki ndiyo cha kutafuta mwafaka,” amesema.
Dk Mbunda amesema maridhiano ni bora zaidi kwani yatapunguza mihemko ya watu kuandamana.
Mchambuzi wa siasa, Magabilo Masambu, ameshauri Serikali kutotumia nguvu kusaka suluhu bali kuwe na mazungumzo.
“Bado muda upo, Serikali isichague kutumia nguvu katika kutatua matatizo. Bado nafasi ipo, yanayolalamikiwa yafanyiwe kazi kwa njia ya mazungumzo,” amesema.
Amesema si lazima Serikali itafutie majawabu changamoto zote zinazolalamikiwa, bali zitafutwe zile zinazogusa wadau wengi.
Mtaalamu wa masuala ya siasa, Florian Karubaga, amesema kinachoendelea nchini kwa sasa si mgogoro wa wananchi na Serikali, bali ni mvutano wa kisiasa kati ya viongozi wa vyama.
“Muhimu ni wananchi kuelewa tofauti kati ya mivutano ya kisiasa na ile ya maendeleo ya jamii. Kuachia wanasiasa kumaliza tofauti zao bila kuwashirikisha wananchi katika maandamano au migongano isiyo na tija,” amesema.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Said Miraji, amesema hoja iliyopo ni kuhusu uwazi wa maandamano hayo yanayozungumzwa mitandaoni, ni nani hasa anayeyaandaa na kwa malengo gani.