Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema Serikali atakayoiunda itawajengea wakulima taaluma, kuwapatia mafunzo ya kisasa na kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje ili waondokane na utegemezi na umaskini uliokithiri.
Othman ametoa ahadi hiyo leo, Alhamisi, Oktoba 16, 2025, alipozungumza katika mkutano maalumu wa wazee wa Shengejuu, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni za urais.
Amesema Serikali yake itawajengea uwezo maofisa wa kilimo ili wawe chachu ya maendeleo vijijini, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuwainua wakulima.
Kupitia mpango huo, amesema maofisa hao watakuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wakulima, kuhakikisha teknolojia mpya za kilimo zinawafikia wananchi moja kwa moja.
Ameeleza kuwa Serikali ya ACT-Wazalendo imejipanga kuboresha kilimo, kikiwemo cha mbogamboga na mazao mengine ya chakula, ili kiwe chanzo kikuu cha mapato kwa wananchi wa Pemba.

Amesema lengo ni kuhakikisha wakulima wanafanya shughuli zao wakiwa na uhakika wa kipato, elimu ya kitaalamu na mazingira rafiki ya uzalishaji.
Amesisitiza kuwa Serikali itawajengea wakulima taaluma, kuwapatia mafunzo ya kisasa na kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Hii itawawezesha wakulima kuondokana na utegemezi na umaskini uliokithiri. Tutahakikisha kila baada ya muda fulani wataalamu wa kilimo Zanzibar wanapewa nafasi ya kujiendeleza kielimu,” ameeleza.
Baada ya elimu kwa wataalamu, amesema Serikali yake itaunda kampuni maalumu ya kilimo itakayoshirikiana nao kwa karibu, ili iwe daraja kati ya Serikali na wananchi, kuhakikisha kila mkulima anafaidika moja kwa moja na jitihada za kitaifa za maendeleo.
Sambamba na ajenda ya kilimo, mgombea huyo amegusia mabadiliko ya tabianchi, akieleza mpango kabambe wa Serikali yake kupima maeneo yote ya Zanzibar ili kubaini yaliyo hatarishi.
“Serikali itawaleta wataalamu wa mazingira kupima ardhi na maji kwa upana wake, ili kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikiathiri uzalishaji katika kilimo,” amesema.
Amesema wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara kutokana na mashamba yao kuharibiwa na mafuriko au ukame, jambo linaloweza kudhibitiwa endapo Serikali itapanga kwa umakini mikakati ya muda mrefu.
Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wazee waliohudhuria, Ali Haji, amesema kauli hizo zinawapa matumaini akisisitiza umuhimu wa utekelezaji iwapo watampa ridhaa.
“Tumekuwa tukisikia ahadi nyingi, lakini hii ya kuwekeza kwenye kilimo cha kisasa na masoko ni ya kweli na inagusa maisha yetu moja kwa moja,” amesema.
Kwa upande wake, Khamis Hassan amesema iwapo ahadi hizo zitatekelezwa, wananchi visiwani humo wataishi maisha bora zaidi ya sasa.