MENEJA Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev, amesema wakati anaendelea kuiimarisha timu hiyo kwa kushirikiana na Kocha Seleman Matola, kuna kitu bado hakijakaa sawa.
Pantev amelitaja eneo hilo kuwa ni la ushambuliaji akisema wanapamba kuhakikisha linakuwa makini katika kutengeneza na kutumia nafasi ili kufunga mabao ya kutosha. Hata hivyo, amesema pia wanajiimarisha kuwa vizuri katika kupishana na mpinzani.
Raia huyo wa Bulgaria, ametoa kauli hiyo wakati Simba ikikabiliwa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini itakayochezwa Jumapili Oktoba 19, 2025.
Simba tayari imefika Eswatini kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Somhlolo ambapo leo asubuhi Oktoba 16, 2025 kikosi hicho kiliondoka jijini Dar.
“Kikosi kipo tayari, kisaikolojia na kimwili, tunafahamu malengo yetu tukiwa tunakwenda kule ambayo ni kushinda mechi hii, tutakuwa na siku kama mbili tatu za mazoezi kurekebisha baadhi ya sehemu zenye upungufu, lakini kwa sasa kikosi kipo tayari.
“Hatuangalii eneo moja pekee, tunachopaswa ni kuwa makini mwanzo hadi mwisho wa mechi kuwa imara katika ulinzi, ushambuliaji na kupishana, tuna mikakati yetu ya kiufundi, nadhani tuna timu nzuri kwa mchezaji mmojammoja na kwa ujumla, kwa hiyo naamini tutashinda mechi hii,” amesema Pantev.
Akizungumzia mikakati aliyoiweka kwa ajili ya mechi hiyo, Pantev ambaye anasaidiana na Seleman Matola kuisuka Simba, amesema: “Tunajaribu kuimarisha maeneo tofauti ikiwamo kumiliki mpira, kujiamini na kutembea na matukio lakini sanasana tunaimarisha eneo la mbele ambalo lazima liwe makini kwa sababu timu ikitengeneza nafasi nyingi kunakuwa na nafasi kubwa ya kufunga mabao.”
Simba katika mechi tano za mashindano ilizocheza msimu huu, imefunga mabao nane, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.
Katika mechi hizo, ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga katika Ngao ya Jamii, kisha ikaichapa Gaborone United bao 1-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Ziliporudiana, matokeo yalikuwa 1-1.
Katika Ligi Kuu Bara, Simba imezifunga Fountain Gate 3-0, kisha ikapata ushindi kama huo dhidi ya Namungo.