:::::::::
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya umeme katika Jiji la Dar es Salaam ambapo ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kuimarisha huduma ya upatikanaji wa umeme ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii.
Mhe. Chalamila amefanya ziara hiyo leo Oktoba 16, 2025 ambapo ametembelea Kituo cha kupoza umeme cha Ubungo, Mradi wa Kituo cha kupoza umeme cha Mabibo na kuhitimisha katika Mradi wa uboreshaji wa njia ya umeme wa msongo mkubwa kutoka Kituo cha kupoza umeme Gongolamboto hadi Kituo cha kupoza umeme Mbagala
Akizungumza wakati wa ziara hiyo katika Kituo cha kupoza umeme Ubungo ambacho kimeongezewa uwezo kwa kusimika Mashine umba ya MVA 300 kutoka MVA 150 ya awali, Mhe. Chalamila ameipongeza TANESCO kwa utekelezaji wa miradi ya umeme kwa ufanisi ambayo imefanikisha kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa anaouongoza.
“Kwa kweli niwapongeze TANESCO kwa mageuzi makubwa. Miezi michache hapo nyuma watanzania wengi walikuwa wanalalamika kukatika kwa umeme lakini leo nikienda kwenye mikutano ya hadhara kila anayeniuliza swali analenga mambo mengine na sio suala la umeme, hizi ni jitihada kubwa zinazofanywa na Shirika. TANESCO ya sasa sio ya jana,’’amesisitiza Mhe. Chalamila
Katika mradi wa Kituo cha kisasa cha kupoza umeme Mabibo ambacho mpaka sasa kimefikia asilimia 71.5 ya utekelezaji wake Mhe. Chalamila amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika kutunza na kulinda miundombinu ya umeme huku akiwataka wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu hiyo.
Akizungumza juu ya umuhimu wa Kituo cha kupoza umeme cha Ubungo Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange amesema kituo hicho kina uwezo wa kupokea umeme kutoka Kituo cha kufua umeme cha Bwawa la Julius Nyerere ambao unapita Kituo cha Chalinze hadi Ubungo lakini pia kinapokea umeme kutoka katika Kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imelenga kukagua maendeleo ya Kituo cha kupoza umeme cha Ubungo, mradi wa Kituo cha kisasa cha kupokea na kupoza umeme cha Mabibo pamoja na mradi wa uboreshaji wa njia ya umeme msongo mkubwa kutoka Kituo cha kupoza umeme Gongolamboto hadi Kituo cha kupoza umeme Mbagala ili kupata mwelekeo wa hali ya upatikanaji wa umeme katika Jiji hilo ambalo ndilo kitovu cha biashara nchini.