Samia aahidi ujenzi Machinga Complex Bukoba

Bukoba. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kujenga jengo kubwa la kisasa la Machinga Complex mjini Bukoba, mkoani Kagera, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya serikali yake ya kuwainua kiuchumi wafanyabiashara wadogo maarufu Machinga.

Akizungumza leo Alhamisi, Oktoba 16, 2025, katika mkutano wa mwisho wa kampeni za CCM kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa uliofanyika katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Mjini, Samia amesema serikali imetenga Sh10 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo katika eneo la Kishenye.

“Ninafahamu changamoto wanazokabiliana nazo ndugu zetu machinga, hasa ukosefu wa maeneo maalumu ya kufanyia biashara. Ndiyo maana tumeamua kujenga Machinga Complex kubwa Bukoba Mjini ili kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira bora na salama,” amesema Samia.

Aidha, ameahidi kuendelea kuboresha sekta ya maendeleo ya jamii, hasa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.

Samia amesema serikali ya CCM imefanya maboresho makubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, ikiwamo kuanzishwa kwa huduma za kibingwa ambazo zimepunguza mahitaji ya wagonjwa kusafiri hadi Bugando au Muhimbili.

“Idadi ya wagonjwa wanaotibiwa hospitalini hapo imeongezeka kutoka 128,305 mwaka 2021 hadi 478,002 mwaka huu. Wote hawa wangehitaji kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo, lakini sasa wanapata huduma ndani ya mkoa wao,” amesema.

Ameongeza kuwa katika miaka mitano ijayo, serikali itaendeleza uwekezaji katika sekta ya afya sambamba na utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote, huku akiahidi kuajiri watumishi wa afya 5,000 ndani ya siku 100 za mwanzo wa serikali ijayo.

Akizungumzia masuala ya maendeleo mengine, Samia amesema serikali itaendelea kuimarisha sekta za kilimo, uvuvi, maji, umeme, elimu na miundombinu ya barabara, akibainisha kuwa miradi mingi tayari imeanza kutekelezwa na malengo ni kuiongezea thamani.

Kuhusu sekta ya umeme, amesema serikali inajenga vituo vipya vya kupooza na kusambaza umeme mkoani Kagera ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa saa 24 bila kukatika, isipokuwa wakati wa matengenezo ya mitambo.

Akizungumzia bandari, mgombea huyo wa urais amesema serikali imeanza maboresho makubwa katika Bandari ya Kemondo kwa kuongeza urefu wa gati na kupanua lango la meli ili kuruhusu meli kubwa kama MV Mwanza, kupakia na kushusha mizigo.

“Lengo letu ni kuwezesha meli kubwa za mizigo na abiria kutia nanga Kemondo. Mamlaka ya Bandari inamiliki ekari 100 kwa ajili ya kujenga miundombinu muhimu kama maghala, huku Bandari ya Bukoba nayo ikifanyiwa marekebisho makubwa,” amesema.

Kuhusu elimu, Samia amesema serikali inajenga tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mkoani humo pamoja na vyuo vya Veta ili kuzalisha wataalamu watakaosaidia kuongeza tija na kipato kwa taifa.

“Tunaendelea kuongeza madarasa na mabweni, hasa katika maeneo ya visiwa ambako wanafunzi wanapata changamoto za usafiri. Tunajenga sekondari na mabweni ili kuhakikisha watoto wanasoma kwa mazingira rafiki,” amesema.

Akihitimisha hotuba yake, Samia amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni na kueleza kuwa huo ni ushahidi wa uungwaji mkono mkubwa kwa CCM.

“Watu ndiyo mashahidi wa Mungu. Walivyotupokea kwa wingi kote tulikopita ni ishara kwamba wana imani na CCM. Tukipata ushindi mkubwa, hakuna wa kulalamika maana watu wenyewe wameshuhudia,” amesema Samia.

Tanzania yauza tani 80,000 sukari nje ya nchi

Waziri wa Kilimo na mgombea ubunge wa Jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema Tanzania imeweka historia kwa mara ya kwanza kuuza nje ya nchi zaidi ya tani 80,000 za sukari, hatua iliyoiingizia Serikali zaidi ya Dola72 milioni  za Marekani (Sh176.4 bilioni).

Bashe amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia katika kuboresha sekta ya uzalishaji wa sukari nchini.

Amesema miaka miwili iliyopita Rais Samia alikipa kiwanda cha sukari cha Kagera eneo la kuongeza mashamba ya miwa, jambo lililoongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 90,000 kwa mwaka aliposhika madaraka hadi kufikia tani 150,000 kwa sasa.

“Kwa kasi hii, ndani ya miaka miwili ijayo, Mkoa wa Kagera utaongoza kwa uzalishaji wa sukari nchini,” amesema Bashe, akibainisha kuwa uchumi wa mkoa huo unategemea kilimo cha miwa, kahawa, mpunga, vanila na tumbaku.

Bashe ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee, serikali imefanikisha mapinduzi makubwa katika sekta ya sukari.

“Maamuzi yaliyofanywa na Serikali mwaka mmoja uliopita yamewezesha sekta ya sukari kuhudumia Watanzania kwa ufanisi. Leo sukari haizidi Sh2,800 kwa kilo, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo bei ilikuwa juu zaidi,” amesema Bashe.

Amefafanua kuwa mafanikio hayo yametokana na upanuzi mkubwa wa mashamba ulioratibiwa baada ya Rais Samia kutoa ardhi miaka miwili iliyopita, ambapo mashamba yote yamepandwa miwa tayari.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Johnson Mutasingwa amesema mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

“Tulikuwa na changamoto ya soko, lakini umetutengea Sh40 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa soko kuu la Bukoba. Pia unajenga stendi kuu, barabara ya kilometa 10.3 na taa za barabarani 413,” amesema.

Mutasingwa ameongeza kuwa Serikali imetenga Sh12.1 bilioni kwa ujenzi wa barabara ya njia nne na Sh19.5 bilioni kwa upanuzi wa Bandari ya Bukoba, ambayo sasa imekamilika na inatumika, ikiwa imepokea meli kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 1,200 pamoja na mizigo.

Aidha, amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo sasa inatoa huduma, huku akiomba hospitali ya mkoa ipandishwe hadhi kuwa ya rufaa kutokana na idadi kubwa ya wananchi wa Bukoba wanaoitegemea.

Naye Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Dk Bashiru Ally amempongeza mgombea huyo wa CCM  kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya na Serikali yake katika sekta ya elimu, hususan maboresho ya mitalaa na mfumo wa mafunzo ya ufundi.

“Nipongeze kwa muundo mpya wa elimu uliolenga kukuza ujuzi na uwezo wa kujitegemea kwa vijana kupitia vyuo vya VETA na vya ufundi,” alisema Dk Bashiru.

Ameongeza kuwa Oktoba 29, 2025 Watanzania watapima uongozi kupitia kura, ambapo mgombea wa CCM atapiga kura Chamwino, Dodoma, akisubiri matokeo akiwa huko.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekiah Wenje  ambaye sasa amehamia CCM, amewaomba  Watanzania kudumisha amani wakati wa kampeni na uchaguzi mkuu.

“Hakuna chama kikubwa kuliko nchi. Ni muhimu kulinda amani na kujitokeza kupiga kura badala ya kufanya maandamano,” amesema Wenje.