SAUT yatoa neno kutoonekana Padre Nikata, yasisitiza uchunguzi wa Polisi

Mwanza. Siku takribani nane tangu taarifa za kutoonekana kwa Padre Camilius Nikata wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea zianze kusambaa na kuibua mshtuko, hatimaye Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) kampasi kuu ya Mwanza kimetoa taarifa kwa umma kuelezea tukio hilo.

Padre Nikata anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na taarifa zake kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya taarifa iliyotolewa na Baba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Mhashamu Askofu Damian Dallu Jumatano Oktoba 8, 2025.

Katika taarifa kwa umma ilitolewa na kusainiwa na ofisi ya uhusiano na mawasiliano- SAUT Oktoba 13, 2025 na kuchapishwa kwenye kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya chuo hicho leo Oktoba 16, 2025 ikiwa na kichwa cha habari ‘Kutoonekana kwa Mfanyakazi wa Chuo, Padre Camilus Nikata’, chuo hicho kimesema kimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kupotea kwake.

Taarifa hiyo imethibitisha kuwa Padre Camilius Nikata ni mfanyakazi wa chuo hicho akiwa ni Mhadhiri katika Idara ya Mawasiliano ya Umma na alikwenda Dodoma kwenye mafundisho.

“Kwa namna ya kipekee uongozi wa SAUT unapenda kuuhabarisha umma kuwa Padre Camilus Nikata ni Mhadhiri wetu katika Idara ya Mawasiliano ya Umma na alikwenda Dodoma kwenye Mafundisho ya Moyo ya mapadre wanaofundisha katika vyuo vikuu vya Kikatoliki nchini vilivyo chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kama ilivyoeleza taarifa ya Baba Askofu Mkuu Damian Dallu,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imetoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi wa kina kumtafuta Padre huyo kwani juhudi zote za kawaida kumtafuta hazijazaa matunda.

“Ofisi ya Baba Askofu Mkuu ilichukua jukumu la kulitaarifu Jeshi la Polisi nchini kwa ajili ya uchunguzi baada ya juhudi zote za kumtafuta kufanyika bila ya mafanikio,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, chuo hicho kimeandaa sala maalumu ya kumuombe Padre Nikata ili apatikane akiwa salama.

“Kufuatia tukio hili la kutoonekana kwa Mhadhiri wetu, Chuo Kikuu SAUT–Mwanza kupitia ofisi ya Chaplaincy imeandaa sala maalumu kwa ajili ya kumuomba Mwenyezi Mungu kumkinga na maovu yote, kumwimarishia ulinzi na kumwongezea usalama Padre Nikata,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya akizungumzia tukio hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari Oktoba 11, 2025 alikiri kupokea taarifa ya kupotea kwa padre huyo na jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kumtafuta.

Kamanda Chilya alisema Padre Nikata alifika Songea Oktoba 3, 2025 akitokea Dodoma akiwa na mhadhiri mwenzake ambaye ni padre wa jimbo la Songea na kufikia katika nyumba ya mapadre St. Shanney.

“llipofika Oktoba 7, 2025 jioni padre Nikata alionekana na padre mwenzake akiwa katika mtaa wa Kanisani barabara kuu akiwa amebeba kibegi kidogo akielekea stendi ya zamani ya mabasi ya Mfaranyaki na kutokea tarehe hiyo hakurudi mahali alipofikia (jimboni),” alieleza Chilya.

Alisema uongozi wa kanisa hilo na mapadre wenzake waliendelea na juhudi za kumtafuta sehemu tofauti ambazo walisadiki kwamba atakuwepo lakini hawakufanikiwa kumpata, ndipo Oktoba 9, 2025 walitoa taarifa ya kutoonekana kwa padre Nikata tangu Oktoba 7, 2025