Musoma. Serikali imetoa zaidi ya Sh5.2 bilioni kwa ajili ya kuwalipa fidia wakazi 58 wa Mtaa wa Bondeni, Kata ya Kamunyonge, Manispaa ya Musoma mkoani Mara ili kupisha mradi wa upanuzi na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma.
Hii ni awamu ya tatu ya ulipaji fidia kwa wakazi wanaozunguka uwanja huo, mradi ambao unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh35 bilioni.
Kukamilika kwa awamu hii kutafanya jumla ya Sh13.2 bilioni kutumika kulipa fidia kwa wakazi 194 wa Kata za Nyasho na Kamunyonge waliokuwa wakiishi karibu na uwanja huo.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka akizungumza wakati wa uzinduzi wa malipo ya fidia kwa wakazi 58 wa mtaa wa Bondeni mjini Musoma kwaajili ya kupisha mradi wa ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
Akizungumza leo Alhamisi, Oktoba 16, 2025, wakati wa uzinduzi wa malipo hayo mjini Musoma, Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Kanda ya Ziwa, Rose Comino amesema malipo hayo yanatarajiwa kukamilika ili kuwapa wakazi hao muda wa kujiandaa kuondoka.
Amesema malipo hayo ni maandalizi ya kuanza kutumika kwa uwanja huo ambao ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 65.
“Tunawalipa wakazi hawa baada ya kuchukua maeneo yao kwa sababu uwepo wao si salama kwa shughuli za uwanja. Lengo letu ni kuhakikisha usalama wa uwanja kwa ujumla,” amesema Comino.
Ameongeza kuwa baada ya malipo, wakazi hao wanatakiwa kuondoka ndani ya siku 45 ili kuruhusu hatua nyingine za mradi kuendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka (katikati) akikabidhi mfano wa hundi kwa baadhi ya wanufaika wa fidia ya Sh5.2 bilioni iliyotolewa na Serikali kwa wakazi wa Mtaa wa Bondeni Manispaa ya Musoma kwaajili ya kupisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
Akizindua rasmi ulipaji huo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema Serikali imetekeleza ahadi yake kwa wamiliki wa viwanja na nyumba waliokuwa wakisubiri fidia baada ya tathmini kukamilika.
Amesema mchakato huo ni suluhisho la changamoto ya muda mrefu iliyowakabili wananchi hao, kwani wengi wao walikuwa na hofu kwamba wangesahauliwa.
“Ni imani yangu kwamba baada ya malipo haya, tutashuhudia matokeo chanya. Mradi huu utawanufaisha wakazi wote wa Musoma kwa kuwa utekelezaji wake unaendelea kwa kasi kubwa,” amesema Chikoka.
Amesema kukamilika kwa uwanja huo kutachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuongeza mzunguko wa fedha na fursa za biashara katika mji wa Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla.

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Bondeni Manispaa ya Musoma wakiwa kwenye uzinduzi wa malipo ya fidia ili kupisha mradi wa upanuzi na ujenzi wa uwanja wa ndege Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
“Watalii na wafanyabiashara wataanza shughuli zao hapa Musoma baada ya kutua uwanjani. Hii itakuza uchumi wa mji wetu na kufungua fursa mpya za maendeleo,” ameongeza.
“Tunaomba tuongezewe muda angalau miezi mitatu ili tupate nafasi ya kutafuta viwanja au nyumba nyingine. Siku 45 ni chache sana,” amesema Laban Ching’oro, mmoja wa wanufaika wa fidia hizo.
Akijibu ombi hilo, Chikoka amesema atalifanyia kazi huku akiwasihi wananchi kuendelea na maandalizi yao wakati mchakato huo ukiendelea.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Bondeni, Emmanuel Baptista amesema malipo hayo yametatua kero iliyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.