Dar es Salaam. Shahidi wa pili wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, amehitimisha ushahidi baada ya kusimama kizimbani kwa siku tano mfululizo.
Shahidi huyo ni Mkaguzi wa Polisi, John Kaaya, kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni, Dawati la Doria Mtandaoni, Makao Makuu wa Polisi, Dar es Salaam.
Amehitimisha ushahidi baada ya Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumaliza kukuuliza maswali ya dodoso kuhusu ushahidi wake wa msingi, alioutoa akiongozwa na mwendesha mashtaka na baadaye kujibu maswali ya kusawazisha majibu yake ya msingi.
Mpaka anahitimisha ushahidi huo leo Oktoba 16, 2025, shahidi huyo ametumia siku tano, moja kwa ushahidi wa msingi na nne za ushahidi wa ziada (yaani akihojiwa maswali ya dodoso na mshtakiwa).
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume cha kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonyesha nia hiyo kwa kuchapisha meneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Katika ushahidi wa msingi pamoja na mambo mengine, shahidi huyo aliieleza mahakama yeye ndiye aliyeiona picha mjongeo (video) katika televisheni ya mtandaoni ya Jambo TV, wakati akifanya doria katika mtandao wa YouTube, Aprili 4, 2025.
Alisema baada ya kuisikiliza aliona katika kauli za Lissu kulikiwa na ujinai, hivyo akamjulisha mkuu wake ambaye alimwelekeza kwa Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam, aliyemwagiza aipakue na ampelekee.
Ifuatayo ni sehemu ya maswali ya kuhitimisha aliyoulizwa na Lissu:
Lissu: Shahidi, nilikuuliza jana kama ulisoma hati ya mashtaka, nataka nikuulize kama tangu jana uliisoma?
Shahidi: Ni sahihi.
Lissu: Hati hii inasema (Lissu anasoma shtaka hilo kama linavyosomeka hapo juu, kisha anamuuliza shahidi kama hayo maneno anayotuhumiwa nayo yako kwenye video?
Shahidi: Ni sahihi, ni sehemu ya mambo uliyochapisha mitandaoni.
Lissu: Kwa hiyo ili kujua maana ya maneno kuchapisha inabidi tuangalie Sheria ya Makosa ya Mitandaoni, kweli au si kweli?
Shahidi: Tunaweza kupata maana kama unavyosema kupitia sheria ya mitandao na sheria nyingine.
Lissu: Ninavyojua mimi ni Sheria ya Makosa ya Mitandaoni?
Shahidi: Nimesema na sheria nyingine kama zipo.
Lissu: Wewe unazijua hizo sheria nyingine?
Shahidi: Nitajikumbusha kama nitakumbuka.
Lissu: Sasa twende kwenye Sheria ya Makosa ya Mitandaoni na angalia kifungu cha 3, waeleze majaji kama kwenye kifungu hicho kuna neno nilaosema uttering (kutamka)
Shahidi: Kuna neno linasema offering words…
Lissu: Nimesema uttering.
Shahidi: Neno uttering halipo.
Lissu amesoma maneno publishing, distributing, transmitting, disseminating, circulating, delivering, exhibition uttering, printing, copying, selling offering, for selling, making on hire or offering to kisha akamuuliza shahidi kama yapo na kumtaka shahidi ayasome. Naye akayasoma.
Lissu: Baada ya kusoma waambie majaji hiyo video iliyoko huko Jambo TV nani aliiweka?
Lissu: Naomba uwaeleze majaji kama mimi nilikuwa na nywila ya kuingia huko.
Shahidi: Sina uhakika kama ulikuwa nayo.
Lissu: Waeleze majaji nani aliye distribute (aliyesambaza) hiyo video maana ilirushwa mubashara.
Shahidi: Ni wewe kupitia Jambo TV.
Lissu alimuuliza shahidi akirejea maneno yote yaliyotajwa katika kifungu cha tatu cha Sheria ya Makosa ya Mitandaoni, kuwa ni nani aliyeyafanya na shahidi huyo akajibu kuwa ni yeye (Lissu) kupitia Jambo TV na mengine akijibu kuwa ni Jambo TV na Tundu Lissu.
Lissu: Ni nani aliyefanya exchange kubadilisha kutoka Jambo TV kwenda Arusha One, TV Clouds, The Chanzo?
Lissu: Nani aliyefanya printing?
Shahidi: Sifahamu (kwa sauti ya chini).
Lissu: Usinong’one.
Shahidi: Hiyo printing sikufuatilia (kwa sauti).
Lissu: Umesema aliyefanya hayo yote ni mimi, waeleze majaji kama mimi nilikuwa na uwezo wa kuingia website ya Jambo TV na kufanya yote hayo.
Shahidi: Hilo Sifahamu.
Lissu: Kama hufahamu yote hayo utawezaje kuwaeleza majaji kwamba ni mimi?
Shahidi: Kitendo cha kuita waandishi wa Jambo TV na kutoa maudhui ulikuwa na nia ya kuchapisha maudhui yako hayo.
Lissu: Kwenye haya yote uliyoyasoma kwenye hii maana (maana ya neno publishing kwenye Sheria ya Makosa ya Mitandao) kuna neno kwamba ukialika watu waje kwenye mkutano kama huo unakosea? yaani kwenye tafsiri ya publishing kuna neno invitation?
Shahidi: Making available.
Lissu: Aah! mwanasheria unadhani digrii zinapatikana kirahisi hivyo kwa kwenda kusomea miezi mitatu kwenye chuo cha JR. Kwenye ushahidi wako nimekuuliza idadi ya watu uliosema waliitazama na waliotoa maoni, swali langu ni kama tangu nimekuliza maswali hayo umepata fursa ya kuangalia tena idaidi ya watu ambao hadi sasa wame-comment (wametoa maoni) kwenye hiyo video iliyoko Jambo TV?
Shahidi: Bado sijapata.
Lissu: Na bado ni msimamo wako kwamba tangu tarehe 4 mpaka sasa hiyo video ina comment 300?
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama ukiwa kizimba hapo umetoa kielelezo chochote kinachothibitisha idadi hiyo ya watazamaji na walio –comment?
Shahidi: Kielelezo bado sijatoa.
Lissu: Sina zaidi kwa shahidi huyu.
Baada ya Lissu kumaliza kumhoji shahidi huyo maswali ya dodoso, mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga naye alimhoji shahidi huyo akimwongoza kufafanua majibu kwa baadhi ya maswali ya dodoso alipohojiwa na Lissu.
Baada ya shahidi huyo wa pili kuhitimisha ushahidi wake, wa tatu wa upande wa mashtaka ameanza kutoa ushahidi wake.
Shahidi huyo ni Mkaguzi wa Jeshi Polisi, Samweli Kahaya (39), mtaalamu wa picha kutoka Kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawab Issa, amezungumzia ajira yake ndani ya Jeshi la Polisi, elimu, ujuzi na taratibu za kazi yake.
Amesema kitengo anachofanyia kazi kinajishughulisha na kupinga na kurekodi picha za mnato na za mjongeo za matukio ya uhalifu, watuhumiwa wa uhalifu na kunafanya uchunguzi wa picha mjongeo na picha mnato, ambalo ndilo jukumu lake.
Pia ameieleza mahakama kwamba ndiye aliyepokea na kufanyia uchunguzi wa kisayansi video ya Lissu pamoja na mambo mengine ili kujiridhisha kama ni halisi au la.
Baada ya maelezo hayo wakati anataka kuingia kwenye ushahidi wa msingi hususani matokeo ya uchungzi wake, Jaji Ndunguru ameahirisha kesi hiyo kutokana na muda kuwa umekwenda ili shahidi huyo aanze rasmi ushahidi kesho Oktoba 17, 2025.