UCHAMBUZI WA DANIEL MJEMA: Mtazamo kupiga kura kishabiki, bendera fuata upepo

Kama wengi wetu tunavyofahamu, Oktoba 29,2025 ndio siku ambayo taifa letu litafanya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani lakini natamani wale wenye sifa ya kupiga kura, tusipige kura kwa ushabiki ama bendera fuata upepo.

Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofaywa Tanzania na wananchi.

Ukisoma Ibara ndogo ya (2) imeweka masharti yanayoweza kuzuia raia asitumie haki yake hiyo kuwa ni pamoja na kama ana uraia wa nchi nyingine, ana ugonjwa wa akili ama ana kumbukumbu ya kutiwa hatiani kwa makosa fulani ya jinai.

Sharti lingine ni kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura, na ukiacha sababu hizohakuna sababu nyingine yoyote inayoweza kumzuia raia asitumie haki ya kupiga kura.

Mbali na Katiba, lakini ukisoma kifungu cha 129 cha sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya 2024, imeharamisha kitendo chochote cha kumshawishi au kumlazimisha mpiga kura huyo kupiga kura au kuacha kupiga kura.

Sheria hiyo inaenda mbali na kukataza mtu yeyote kumzuia mpiga kura asitumie haki yake kwa kwa kumteka nyara, vitisho au hila ya aina yoyote, na akifanya hivyo basi anatenda kosa la ushawishi mbaya kwa maana ya Sheria hiyo.

Ninayasema haya kwa sababu tayari huko mitaani kuna vuguvugu la makundi matatu, wapo ambao “Oktoba wana tick (kuweka vema)” na lipo kundi linalohamasisha watu wasipige kura bali washiriki katika maandamano.

Lakini lipo kundi lingine ambalo lenyewe limeamua tu kwamba hawatajitokeza si kwenye kupiga kura bali watabaki nyumbani na kundi hili lina sababu moja tu, kwamba hawana uhakika uchaguzi utakuwa wa huru, haki na unaoaminika.

Sitaki kuzungumzia uamuzi wa waliosusa kwa sababu wana sababu zao na wana haki ya kufanya hivyo, lakini kwa muktadha wa makala hii, nataka nizungumzie kidogo athari za watu kupiga kura kwa kwa ushabiki au bendera fuata upepo.

Kuna kitu kinaitwa “Group Psychology” (saikolojia ya kikundi) huathiri pakubwa tabia ya upigaji kura, kuchagiza jinsi mtu binafsi anavyofanya maamuzi ndani ya kikundi au muktadha wa pamoja na wakati mwingine bila kujali sifa ya mgombea.

Vipo vigezo kama vitano vinavyosababisha Group Psychology navyo ni pamoja na kitu tunakiita “Bandwagon effect” ambayo ni watu huwa wanafuata maoni ya wengi au mwelekeo ambao mara nyingi humpigia kura mgombeaji maarufu zaidi.

Lakini kuna kigezo kingine ambacho ni nadharia ya utambulisho wa kijamii au social identity theory ambapo mtu anaweza kupiga kura kwa sababu tu ya nasaba yake na chama cha siasa au mgombea na si kwa kuegemea sifa ya mgombea.

Mbali na kigezo hicho lakini kuna shinikizo la watu wako wa karibu (peer pressure) ambayo ni ile hamu ya kufuata maoni ya marafiki, familia, au wafanyakazi wenza ama rika mliokua pamoja tangu wadogo inaweza kuathiri maamuzi ya kupiga kura.

Sasa kuna njia tatu za kukwepa kuingia katika mtego wa kuchagua kiongozi kwa ushabiki au bendera fuata upepo na mojawapo ni kuhimiza mitazamo mbalimbali tofauti tofauti kwani kunaweza kusaidia wapiga kura kufanya maamuzi sahihi zaidi.

Njia nyingine ni “Critical thinking” ambayo ni uwepo wa fikra tunduizi ambayo inasaidia kukuza ustadi wa kufikiria kwa kina ambako kunaweza kusaidia wapiga kura kutathmini habari kwa ufanisi zaidi na kupinga shinikizo la kikundi chochote.

Sasa tuna vyama 18 vinashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025 kikiwepo Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuna aina mbili za upigaji kura, moja ni perfomance voting (kwa kupima ufanisi) na mbili, ni promise voting kwa ahadi.

CCM kwa sababu ndio chama tawala kitapigiwa kura kwa njia zote mbili, kwanza wapiga kura wanapaswa kukipima kama kimetekeleza ilani yake ya 2020-2025 kwa ufanisi kiasi gani, halafu sasa watakipima kwa ahadi watakazozitoa.

Vyama vya upinzani na wagombea wao, wao watachaguliwa kwa kigezo kimoja tu nacho ni “promise voting” kwamba wapiga kura watasikiliza ilani na ahadi za wagombea na kuzipima kisha kuamua kama wanafaa kupewa ridhaa ya uongozi.

Sasa haya yote yanaweza yasiwe na maana kama wapiga kura wenyewe hawafuatilii ilani za vyama wala ahadi za wagombea wanazozitoa, na ikitokea hivyo maana yake watafanya maamuzi kwa ushabiki au bendera fuata upepo.

Hili likitokea lina hatari sana kwani tunaweza kujikuta kama taifa, tuna viongozi wasio na sifa na mwisho wa siku hata serikali inayoundwa inakuwa legelege na isiyoweza kuwaongoza watanzania kufikia nchi ya asali na maziwa.

Tusichague kiongozi kwa kutizama eti kwa kuwa ni mtoto wa mjomba, nimesoma naye au amenipa kilo ya sukari, kitenge, duveti ama fulana, hapana, tuwapime wagombea kupitia vigezo mbalimbali ikiwamo ilani zao na ahadi zao majukwaani.

Ninatamani tuchague kiongozi bora na si bora kiongozi na nia pekee ya kuwafahamu ni kupitia wasifu wao, historia zao na ilani za chama na ahadi binafsi majukwaani, kwani hizo ndio zinapaswa kutumika kupima ubora wa mgombea.

Vyombo vya Habari vinapaswa kutoa nafasi sawa kwa wagombea hasa wa kiti cha urais, ili wapiga kura wapige kura wakiwa informed (wanajua) nini kinatofautisha kati ya mgombea mmoja na mwingine au sera ya chama kimoja dhidi ya kingine.

Ingekuwa ni amri yangu, ningechagua mtu badala ya chama kwa sababu tukiegemea kuchagua chama badala ya mtu ndio tunarudi kule kule kwenye group psychology ambayo inaweza kutupa kiongozi asiye na sifa ya kuwa kiongozi.

Mwigizaji raia wa Marekani, Nikki Reed anasema “Dont just vote. Know what you are voting for, and stand by that”, akisema ni muhimu usipe kura tu ilimradi kupiga, ni lazima ujue kwanini unapiga kura, nami nasema tusipige kura kimkumbo mkumbo.