Dar es Salaam. Umati wa wananchi wa Kenya, umefurika katika barabara mbalimbali unakopitishwa mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga.
Kwa maelfu ya wananchi waliojipanga barabarani, baadhi wakiangua vilio kwa majonzi, ulitosha kuashiria kuwa, Odinga ni miongoni mwa wanasiasa waliokuwa mioyoni mwa watu.
Odinga alifariki dunia jana Oktoba 15, 2025 nchini India, alikokuwa anapatiwa matibabu.
Wingi wa wananchi waliojitokeza kusindikiza mwili wake, umesababisha Serikali ibadili ratiba, badala ya kuupeleka nyumbani, utapelekwa Uwanja wa Moi Kasarani kutoa nafasi kwa wafuasi wake na wananchi kutoa heshima za mwisho.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Serikali ya Kenya, mwili wa Odinga, utapitishwa Makafani ya Lee kisha Uwanja wa Moi Kasarani.
Mwili wa Raila umepokelewa leo, Alhamisi Oktoba 16, 2025 na idadi kubwa ya wananchi waliosababisha kusimama kwa shughuli katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), baadhi wakiingia ndani ya ndege iliyobeba mwili.
Licha ya ulinzi mkali uliokuwa umeimarishwa katika uwanja huo, wingi wa wananchi uliwazidi hadi wanajeshi na kulifikia jeneza lililokuwa na mwili wa Raila, huku wakiomboleza bila kikomo.
“Ni baba pekee ndiye anaweza kutuliza. Aamke atutulize,” zilisikika sauti za baadhi ya waombolezaji wakiwa katika uwanja huo kuupokea mwili wa Odinga.
Rais William Ruto, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, familia ya marehemu Raila, viongozi wa Serikali na wanasiasa mbalimbali waliofika kuupokea mwili huo, hawakupata nafasi kwa sababu ya umati uliokuwepo.
Msafara wa Rais Ruto na viongozi wengine ulibaki JKIA, kisha baadaye ukafuata ule ambao umebeba mwili wa Odinga ambao bado upo njiani kuelekea Lee.
Baadhi ya wafuasi wa Odinga, wameapa lazima waongoze na kuelekeza ratiba ya kuagwa kwake. Katikati ya Jiji la Nairobi, kila aliyetembea kitu chochote kuashiria kuomboleza huku pikipiki na magari yakipiga honi.
Haya yanafanyika huku wakazi wa Kisumu nao wakisubiri kwa hamu na kuupokea mwili wa shujaa huyo afike nyumbani kwake.
Raila atazikwa Jumapili hii, mazishi ambayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wengi ndani na nje ya nchi.
Shughuli katika Uwanja wa JKIA, zilisitishwa kwa muda baada ya waombolezaji kuvuruga usalama humo mwili wa Odinga ulipokuwa ukiwasili.
Mamlaka ya Kusimamia Safari za Angani (KCAA), ilieleza ililazimika kuchukua hatua hiyo baada ya waombolezaji kuingia sehemu zisizoruhusiwa katika uwanja huo.
“KCAA inajulisha umma kwamba shughuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta zimesitishwa kwa muda kutokana na hali ya usalama iliyoshuhudiwa kufuatia kufika kwa mwili wa Raila Odinga,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa KACC Emile Arao.
Mamlaka hiyo imetoa wito kwa umma na wasafiri kubaki watulivu na kutofika katika uwanja huo wa ndege hadi mwelekeo utakapotolewa baadaye.
“Shughuli za kawaida zitarejea baada ya Uwanja wa JKIA kutangazwa kuwa salama,” amesema Arao.
Ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) iliyobeba mwili wa Odinga ilipowasili katika uwanja huo, maelfu ya waombolezaji walionekana kuwazidi nguvu maofisa wa vikosi mbalimbali vya usalama.
Isitoshe, baadhi yao, waliokuwa wakilia kwa sauti wakibeba matawi, walionekana karibu zaidi na ndege hiyo.
Kando na hayo, shughuli za kijeshi zilizoratibiwa kufanyika katika uwanja wa JKIA wakati wa kupokewa kwa mwili huo pia zilifutiliwa mbali.
Eneo la salamu za mwisho labadilishwa
Eneo lililopangwa kwa wananchi kutoa salamu za mwisho kwa mwili wa kiongozi huyo limebadilishwa kutoka Bunge la Kitaifa hadi Kasarani.
Hiyo ni baada ya wafuasi au waombolezaji kujaa bungeni wakisubiri kutazama mwili wa kiongozi huyo mashuhuri.
Wale ambao tayari walishapanga foleni bungeni wameshauriwa kuelekea kwenye Kituo cha Michezo cha Kimataifa cha Kasarani.
Barabara ya Thika Road imefurika umati na magari watu wakielekea Kasarani.