Urais wa Mpina ndio basi tena!

Dodoma/Dar. Ni mwisho wa safari ya Luhaga Mpina kusaka urais? Ni swali linalogonga vichwa vya wengi kwa sasa baada ya Mahakama Kuu kuitupa kesi ya kikatiba, aliyofungua yeye na bodi ya Wadhamini wa ACT-Wazalendo dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Wakati mahakama ikiitupa kesi hiyo, leo Oktoba 15, 2025, chama hicho kimetoa taarifa kwa umma kikisema kitachukua hatua zaidi za kisheria ikiwa ni pamoja na kukata rufaa mahakama ya juu zaidi kupinga uamuzi huo.

Lakini kupitia taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo, chama hicho kimeeleza kitawashirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi na kuendelea kupigania mabadiliko ya kikatiba na kisheria kwenye uchaguzi.

ACT-Wazalendo imewataka wafuasi na wanachama wake kuwa watulivu, wamoja na kujielekeza kwenye uwanda mpana wa mapambano ya demokrasia na haki na kusisitiza kaulimbiu yao ya “Tubaki wamoja na safari inaendelea.”

“Tuliingia kwenye mapambano ya kisheria tukitafuta haki, uwazi na kila mara tumeendelea kusisitiza ushiriki ulio sawa kwenye mchakato wa kidemokrasia ikiwamo uchaguzi,” imeeleza taarifa ya ACT-Wazalendo.

“Hata kama mahakama haikusikiliza maombi yetu kwa muktadha wake (on merit), bado tutaendelea na juhudi za kuitafuta haki na tunu za demokrasia nchini.”

Chama hicho kimeeleza katika hukumu, Mahakama Kuu imetoa uamuzi kwa kujiegemeza kwenye pingamizi za kisheria zilizowekwa na upande wa Serikali juu ya uwezo wa Mahakama kusikiliza shauri hilo.

Hii ni kutokana na uwepo wa vifungu vinavyotoa kinga kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa uamuzi itakaofanya, ambavyo mahakama imekubaliana navyo, hivyo kuliondoa shauri hilo mahakamani.

Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia hukumu hiyo, Mpina amejibu kuwa ameshaipokea hukumu na tayari ameshakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kwa hatua zaidi za kisheria.

“Tumeshapokea hukumu, tumekata rufaa zaidi ni kama taarifa ya chama ilivyosema,” amesema.

Mpina na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho walifungua shauri mahakamani kupinga uamuzi wa kuondolewa katika nafasi ya kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maelezo kuwa uteuzi wake ulikiuka taratibu za chama.

Hukumu ya kesi hiyo namba 24022 ya mwaka 2025 imesomwa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma leo Jumatano Oktoba 15, 2025 na Jaji Fredrick Manyanda aliyekuwa kiongozi wa jopo la majaji watatu waliosikiliza shauri hilo. Majaji wengine ni Sylvester Kainda na Abdallah Gonzi.

Katika hukumu hiyo, Jaji Manyanda ametaja sababu kuu ya kuitupa kesi hiyo ni sheria na Katiba ya nchi kwamba, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) haipaswi kuingiliwa na chombo chochote kwa jambo ambalo ilifanya kwa nia njema.

Kwa uamuzi huo, ni wazi kuwa milango ya kugombea urais 2025 kwa Luhaga Mpina ni finyu labda kama atakata rufaa na kushinda na mahakama kutoa amri kwa INEC kumrudisha kugombea na mchakato wa uchaguzi mkuu kuanza upya.

Kuondolewa kwa Mpina kunafanya wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 kubaki 17 ingawa kwenye nafasi za ubunge na udiwani chama hicho kimeweka wagombea maeneo mengi.

‎‎Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025 kuomba uteuzi wa INEC kupeperusha bendera yake katika uchaguzi huo.

‎Hata hivyo, Agosti 26, Msajili wa Vyama vya Siasa, alitangaza kubatilisha uteuzi wake kutokana na pingamizi lililowasilishwa kwake na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala.

‎Alidai uteuzi wa Mpina ni batili kwani hakuwa na sifa kwa mujibu Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa chama hicho, Toleo la mwaka 2015.

‎‎Monalisa alidai Mpina anakosa sifa zote hizo, kwa kuwa alijiunga na chama hicho, Agosti 5, 2025 na aliteuliwa siku moja baada ya kujiunga, badala ya kusubiri siku 30.

Kutokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, INEC ilitangaza kumwondoa Mpina katika orodha ya walioomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.

Vilevile, INEC ilimtaka Mpina asifike ofisi zake siku ya uteuzi wa wagombea, Agosti 27, 2025 na hata alipokwenda alizuiwa na askari polisi kuingia katia ofisi hizo.

Mpina alianza mapambano ya kisheria, kuanzia tarehe hiyohiyo aliyozuiwa kuingia ofisi za INEC kurejesha fomu yake, kwa kufungua mashauri mawili mahakamani.

Shauri la kwanza lilikuwa la Kikatiba lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa ACT-Wazalendo na Mpina dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo namba 21692 la mwaka 2025 lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, pamoja na mambo mengine walipinga uamuzi wa INEC kumwengua Mpina miongoni mwa wagombea.

Pia, walifungua shauri dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika shauri hilo la maombi namba 23617 la mwaka 2025, Mpina na Bodi ya Wadhamini wa ACT-Wazalendo  waliomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa Msajili kubatilisha uteuzi wake.

Katika uamuzi uliotolewa Septemba 11, 2025 na jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza, mahakama ilitengua uamuzi wa INEC.

Mahakama ilifikia uamuzi huo baada ya kukubali hoja za Mpina kwamba hakupewa haki ya kusikilizwa na INEC wakati ilipomwengua, kinyume cha Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba ya Nchi.

Hivyo, mahakama ilibatilisha uamuzi wa INEC kumwengua Mpina na kuiamuru ipokee fomu zake za kuomba utezi na iendelee na mchakato wa uteuzi wake kuanzia pale ulipokuwa umeishia.

Baada ya hatua hiyo, Mpina alikabidhi fomu na kuteuliwa kuwa miongoni mwa wagombea.

Hata hivyo, Mpina alijikuta akikabiliwa na kikwazo kingine cha pingamizi tatu kuhusu uteuzi wake zilizowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mgombea urais wa Chama cha AAFP na mgombea urais wa Chama cha NRA.

Katika uamuzi wake wa Septemba 15, 2025, INEC ilitupilia mbali pingamizi za wagombea wa AAFP na NRA dhidi ya Mpina, lakini ikakubali la Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo ikatengua tena uteuzi wake.

Uamuzi huo ulisababisha Mpina na Bodi ya Wadhamini ya ACT- Wazalendo kuirudisha INEC mahakamani kwa mara nyingine, ambayo imetupwa leo.

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Dk Matrona Kabyemela amesema: “Tunaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni, kama wameona hawajatendewa haki wanaweza kwenda juu, ni muhimu vyama vya siasa vifuate sheria na kanuni walizojiwekea.”

Kwa upande wake, Profesa Abel Kinyondo, amesema Mpina ajitathmini kama mwanasiasa, akieleza kwa mtazamano wake haiwezekani kuwa mwanachama mpya na kupewa majukumu makubwa ya kugombea urais, kwani tayari ACT-Wazalendo ilikuwa na mgombea.

“ACT-Wazalendo ilikuwa na mgombea Mpina akapewa nafasi hiyo na aliyekuwa mgombea (Dorothy Semu) alijiuzulu, jambo ambalo haiwezekani. Pingamizi la kwanza la kumpinga Mpina asigombee liliwekwa na kiongozi wa chama hicho, tena mwandamizi na si nje ya chama,” amesema.

Profesa Kinyondo anarejea miaka mitano nyuma wakati chama hicho kilipomteua Bernard Membe kugombea urais, akisema hata yeye mgombea alifahamu ACT-Wazalendo haikuwa na nia ya kuchukua nchi kwenye uchaguzi huo, ndiyo maana alifanya mkutano mmoja na kutulia.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Aidan Msafiri amesema kama uamuzi umefanyika kulingana na sheria ni sawa, akisisitiza kila chama au taasisi lazima kifuate utaratibu wake.

“Lakini lipo la kutafakari, uamuzi huu kuna uongo ndani yake, Mpina angekidhi vigezo angepewa nafasi ya kugombea, kuna jambo nyuma ya pazia,” amedai.