Kutokana na hali hiyo, vyuo vya afya vya umma na binafsi, ikiwemo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), vimeshauriwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa fani ya kinywa na meno, sambamba na kuanzisha kozi maalum ya wauguzi wa meno watakaosaidiana na madaktari hao katika utoaji wa huduma.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Afya ya Kinywa na Meno wa Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzobo, wakati wa Kongamano la 15 lililoandaliwa na MUHAS kwa lengo la kujadili na kutoa mapendekezo ya kuimarisha huduma za afya ya kinywa na meno nchini.
Dkt. Nzobo alisema changamoto za kinywa na meno bado ni kubwa, hivyo zinahitaji wataalamu wabobezi na wauguzi wenye ujuzi maalum ili kutoa matibabu kwa viwango vinavyokubalika na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Alifafanua kuwa kwa sasa madaktari bingwa wa kinywa na meno nchini hawazidi 100, wakati uhitaji ukiwa ni madaktari 300. Aidha, madaktari wa shahada ya kwanza wanaohitajika ni takriban 970 na matabibu wa meno 2,600.
“Daktari bingwa anahitaji muuguzi aliyebobea katika huduma za kinywa na meno, lakini kwa sasa hakuna nesi hata mmoja mwenye ujuzi huo nchini. Huu ni wito kwa vyuo vyetu vya afya kuhakikisha vinaanzisha programu za uuguzi katika eneo hili ili waweze kusaidiana na madaktari kutoa huduma bora,” alisema Dk. Nzobo.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, asilimia 76.5 ya watu wazima wana tatizo la kuoza meno, huku kwa watoto tatizo hilo likifikia asilimia 31.1. Aidha, asilimia 68 ya watu wazima wana changamoto za magonjwa ya fizi, na kwa watoto ni asilimia 57, huku asilimia 33.1 ya Watanzania wakikabiliwa na tatizo la meno ya kahawia.
Dkt. Nzobo aliongeza kuwa kumekuwa na ongezeko la watu wanaozibwa meno, kutoka asilimia 10 mwaka 2010 hadi asilimia 42, na kusisitiza kuwa dawa ya jino bovu si kung’oa, bali kutibu kwa kuliziba.
Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali imewekeza Shilingi bilioni 17 katika Idara ya Kinywa na Meno kwa ajili ya kununua mitambo ya kutoa huduma hiyo na kuisambaza katika hospitali za taifa, kanda, rufaa na vituo vya afya.
Fedha hizo zilitumika kununua viti maalum 990, mashine za X-ray 560, na mashine 15 za mionzi za meno (CBCT Scan).
Akifungua kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe, alisema afya ya kinywa ni sehemu muhimu ya ustawi wa mwili mzima, na jamii inapaswa kuelimishwa zaidi kuhusu kupiga mswaki mara mbili kwa siku, kupunguza vyakula vyenye sukari nyingi, na kutembelea madaktari wa meno mara kwa mara.
“Afya ya kinywa mara nyingi imekuwa ikipuuzwa licha ya kuwa sehemu muhimu ya afya kwa ujumla. Inahusiana na ubora wa maisha, heshima ya binadamu na hata uwezo wa kufanya kazi. Afya duni ya kinywa inaweza kuiingiza familia katika changamoto za kifedha, hasa pale ambapo huduma hizo hazijajumuishwa katika mifumo ya huduma za msingi,” alisema Dk. Shekalaghe.
Alibainisha kuwa bima ya afya kwa wote itajumuisha huduma muhimu za afya ya kinywa katika huduma za msingi, ili kila Mtanzania aweze kupata matibabu bila changamoto za kifedha.
“Dawa muhimu za meno zimeanza kujumuishwa kwenye orodha ya dawa, na huduma hizi sasa zinapatikana katika vituo vya afya vya ngazi ya msingi. Hii ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa malengo ya Afya kwa Wote (UHC),” aliongeza.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Emmanuel Balandya, alisema kongamano hilo ni sehemu ya juhudi za chuo hicho kuhakikisha elimu ya afya ya kinywa inakuwa endelevu na inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
“Tunapitia mitaala yetu ili iendane na mabadiliko ya teknolojia. Tunataka kizazi kipya cha wataalamu wa meno wawe na ujuzi wa kidijitali na wawe tayari kuhudumia jamii kwa ubunifu na weledi,” alisema Prof. Balandya.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzobo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la 15 la Afya ya Kinywa na Meno.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya (kushoto) akimkabidhi Zawadi mgeni rasmi wa Kongamano la 15 la Afya ya Kinywa na Meno Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe.