Wabunifu majengo, Wakadiriaji Majenzi wahimizwa kuzingatia ubora

Arusha. Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Miundombinu, Rogatus Mativila amewataka Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kuzingatia kasi ya mabadiliko ya maendeleo ya dunia kwa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora, usalama na uendelevu.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Bodi ya Usajili ya wataalamu hao leo Jumatano, Oktoba 15, 2025 amesema kuzingatia viwango siyo tu kufata kanuni kwa lazima bali ni kufanya kazi kwa weledi kwa kutumia teknolojia na kuweka ubunifu katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi.

Amesema Serikali imeendelea kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya ujenzi zikiwemo barabara za kisasa, madaraja makubwa, hospitali za rufaa, shule za mfano, vituo vya afya, majengo ya utawala pamoja na miradi mingine mikubwa ya miundombinu ikiwemo SGR, Bwawa la Julius Nyerere, vituo vya kisasa vya mabasi na vituo vya huduma za kijamii.

Wataalamu wa sekta ya ujenzi wakiwa kwenye mkutano wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi nchini ukiofanyika leo jijini Arusha.Picha na Filbert Rweyemamu

“Miradi hii yote ni kielelezo cha ushirikiano wa kitaalamu kati ya Serikali na sekta binafsi ,tukitambua ubunifu na ukadiriaji sahihi majenzi ni moyo wa maendeleo wa taifa huku sekta ya ujenzi ikiwa ina nafasi kubwa ya kutafsiri dira ya maendeleo kuwa matokeo yanayoonekana kama barabara, majengo huduma na fursa za ajira,” amesema Mativila.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema kutoka na umuhimu wa sekta ya ujenzi wataalamu hao wanapaswa kuendelea kuwa mabalozi wa uadilifu na uwajibikaji katika miradi yote ya umma na binafsi na kuvitaka vyama vya kitaaluma kuongeza nguvu katika kutoa elimu endelevu, mafunzo ya kimaadili na maadili ya kitaaluma.

“Nawasihii wadau wote ikiwemo serikali, sekta binafsi na taasisi za kifedha kuwekeza zaidi katika ubunifu wa teknolojia kwasababu tunahitaji majengo yanayohimili mabadiliko ya tabia nchi, miradi ya kijani, matumizi ya vifaa vya kisasa na mifumo ya kidijitali katika usanifu na ukadiriaji wa miradi,”amesema Mativila.

Amefafanua kuwa kupitia ubunifu wadau watashuhudia ujenzi wa miji bora, salama na rafiki kwa mazingira inayoendana na ndoto ya Tanzania ya viwanda na uchumi  wa kidijitali jambo litaloipa heshima taaluma hiyo.

Mativila amesema ili sekta ya ujenzi itoe mchango unaostahili kwa taifa Bodi ya Usajili ihakikishe inaboresha mifumo ya usajili na ufatiliaji wataalamu ili kudhibiti matapeli wa taaluma na kampuni zisizo na usajili halali.

Pia, bodi iendelee kutoa programu ya mafunzo endelevu ili kuongeza mafunzo ya wataalamu hasa vijana wanaoingia kwenye soko la ajira na bodi ishirikiane na Wizara ya Ujenzi na Tamisemi kuhakikisha miradi yote ya umma inasimamiwa na wataalamu waliothibitishwa ili kulinda ubora na usalama wa miradi.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali (Tamisemi)-Miundombinu,Rogatius Mativila(katikati)akimkabidhi mwakilishi wa kampuni ya Salebhai Glass Industry,Hilda Bazil mmoja wa wadhamini wa mkutano huo,kushoto ni Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili Majengo na Ubunifu Majenzi,Dk.Daniel Matondo.Picha na Filbert Rweyemamu

Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajiliwa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Dk Daniel Matondo amesema mkutano huo wa sita wa mwaka pamoja na mambo mengine utajikita kujadili mada zinazohusu udhibiti na taratibu wa udhibiti wa miradi na mifumo ua Usalama na afya kazini.

Ametaja mada zingine ni usalama wa moto katika miradi ya ujenzi, uendelevu wa mazingira, tathmini na athari zake, udhibiti wa maadili na sheria pamoja na ufuatiliaji na ripoti za uzingatiaji mahiri.

“Katika kujadili mada hizi tumealika taasisi za udhibiti lengo kuu likiwa kukaa pamoja na kuweza kubadilishana uzoefu katika udhibiti wa sekta ya ujenzi, tunaamini majadiliano yatawezesha kuongeza ufanisi katika udhibiti wa majenzi nchini ili kupunguza mapungufu mbalimbali yanayojitokeza katika sekta hii,”amesema Dk Matondo.

Ameongeza kuwa hadi Septemba 30,2025 Bodi hiyo imesajili wataalamu 1,770 na makampuni 507 na katika kipindi cha Januari hadi Septemba wamefanikiwa kufanya ukaguzi wa majengo na majenzi yaliyosajiliwa awali na yaliyoanza kujengwa yapatayo 4,598 huku ikisajili miradi iliyokidhi mahitaji 1,276 na waendelezaji zaidi ya 103 wamefikishwa mahakamani kwa kutofata taratibu za kisheria.