Akamatwa Tabora kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano, Chacha aonya

Tabora. Kijana mwenye umri wa takriban miaka 30, ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kisheria, amekamatwa na vyombo vya dola mkoani Tabora kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano badala ya wananchi kupiga kura.

Taarifa za awali zinaonyesha kwamba mtuhumiwa aliamsha hofu baada ya kuandika ujumbe kwenye mlango wa nyumba ya mkazi mmoja wa Wilaya ya Nzega, akielekeza wananchi wasihudhurie uchaguzi bali wajitokeze kwa maandamano siku ya Oktoba 29.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Moshi leo Ijumaa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Matiko Chacha, amesema mtuhumiwa yuko mikononi mwa vyombo vya dola na anaendelea kuhojiwa ili kubaini mtandao wake na nia halisi ya uanzishaji wa maandamano hayo.

“Tumemkamata kabisa. Yupo kituoni na anaendelea kuhojiwa ili tuweze kujua ni mtandao upi anashirikiana nao. Tabora tutahakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani; wale wachache wanaotaka kutuvuruga tutashughulika nao,” amesema Chacha.

RC Chacha alisisitiza kuwa mkoa umeimarisha usalama na kwamba vyombo vya ulinzi vimejipanga kuhakikisha wananchi wanachagua viongozi wao kwa amani. Alitoa wito kwa wananchi kupiga kura kwa amani na kurudi nyumbani bila hofu ya vurugu.

“Amkeni mkaende kupiga kura, msiogope chochote. Haiwezekani mtu aje hapa kutusumbua kwa kuhamasisha watu wasipige kura. Tutachukua hatua dhidi ya wale wote watakaofanya fujo,” amesema.

RC Chacha pia alionya kuwa, kuanzia sasa hadi siku ya uchaguzi, mtu yeyote atakayepatikana akaandika au kuweka maandishi kwenye milango au kuta za vyombo vya watu binafsi atachukuliwa hatua; mtuhumiwa anaweza kushikiliwa hadi uchaguzi utakapokwisha na uchunguzi ukikamilika.

Kuhusiana na vitisho vilivyokuwa vikitolewa juu ya kutaka kuchoma vituo vya mafuta siku ya uchaguzi, RC Chacha aliwahakikishia wamiliki wa vituo vya mafuta mkoani humo kuwa hakuna atakayeruhusiwa kufanya hivyo.

“Kuna watu wanazungumza maisha, lakini tuna mfumo wa ulinzi hapa. Wakati wowote watakaojaribu kutekeleza vitisho vitashughulikiwa,” amesema.