Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekanusha taarifa zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa taasisi hiyo imechapisha fedha na kuzisambaza kwa ajili ya kugharamia uchaguzi mkuu, ikieleza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote, ni upotoshaji unaolenga kupotosha umma.
Aidha, katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, na kusainiwa na Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, BoT imesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakihamasishwa kuondoa fedha zao kwenye benki za biashara kwa madai kuwa zinaishiwa fedha kutokana na uchaguzi.
Hata hivyo, BoT imesisitiza kuwa taarifa hizo pia ni za uongo na zinapaswa kupuuzwa na umma.
“Ninapenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa taarifa hizo si za kweli, zinapaswa kupuuzwa na kukemewa wote wanaozisambaza,” imesema taarifa hiyo.
BoT imefafanua kuwa, kama ilivyo katika nchi nyingine duniani, kuchapisha fedha hufanywa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, Sura ya 197, Benki Kuu ina jukumu la kuzungusha kiasi cha fedha kinachohitajika katika shughuli za kiuchumi pamoja na mahitaji ya kubadilisha fedha zilizochakaa.
Aidha, imebainisha kuwa fedha hizo huingizwa kwenye mzunguko kupitia benki za biashara na si vinginevyo, na kwamba mchakato huo hufanyika kwa kufuata taratibu rasmi ili kuhakikisha sera za fedha na utulivu wa bei unadhibitiwa ipasavyo.
BoT imesema imeendelea kutekeleza sera zake kwa ufanisi ili kudhibiti mfumuko wa bei, ambao kwa sasa upo katika wastani wa asilimia 3.3 kwa miezi 10 ya mwaka 2025, ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 6 kwa mwaka mzima.
Taarifa hiyo imesema urari wa malipo kwa taifa unabaki kuwa imara kwa asilimia 2.4 ya pato la Taifa hadi Septemba 2025, huku thamani ya Shilingi ya Tanzania ikiimarika kwa wastani wa asilimia 8.8 dhidi ya Dola ya Marekani katika kipindi hicho.
Vilevile, taarifa hiyo imefafanua kuwa akiba ya fedha za kigeni imeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani 6.7bilioni, zinazotosheleza uagizaji wa bidhaa kwa miezi zaidi ya mitano.
Kupitia taarifa hiyo, Tutuba ameeleza kuwa benki zote nchini zinasimamiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na viwango vya kimataifa vinavyohakikisha zinakuwa na mitaji ya kutosha, ukwasi unaotosha na zinapata faida.
Ameongeza kuwa, takwimu za hivi karibuni (Septemba 2025), zinaonyesha kuwa sekta ya benki imeendelea kuwa imara, ikiwa na kiwango cha mikopo chechefu cha asilimia 3.3 ambacho ni chini ya ukomo wa asilimia 5.
Pamoja na hayo, amesema mifumo ya malipo inaendelea kusimamiwa kwa ufanisi ili kuwezesha miamala yote ya kifedha kufanyika kwa usalama na uwazi, jambo linaloimarisha imani kwa taasisi za kifedha nchini.
Gavana Tutuba amesisitiza kuwa katika mazingira mazuri ya kiuchumi na kifedha nchini, kuondoa fedha benki na kuzihifadhi nyumbani si kitendo cha kiusalama wala cha kiuchumi, bali ni hatua yenye hatari nyingi.
“Uamuzi wa kuondoa fedha benki na kuziweka nyumbani unaweza kusababisha hatari kama vile wizi, upotevu au uharibifu wa fedha. Aidha, fedha hizo hazitazalisha faida wala kuchangia ukuaji wa uchumi,” amesema.
Hivyo, BoT imewakumbusha wananchi kuwa fedha zilizowekwa benki zinaendelea kulindwa kwa usalama, zinapata faida kupitia riba na zinachangia ukuaji wa uchumi kwa kuwezesha upatikanaji wa mikopo inayochochea shughuli za maendeleo.
“Wananchi washauriwe kuendelea kutunza fedha zao benki kwa sababu watapata faida kupitia riba na usalama wa uhakika, huku wakisaidia benki kutoa mikopo kwa wajasiriamali na sekta mbalimbali za kiuchumi,” imefafanua taarifa hiyo.
Gavana Tutuba ametahadharisha kuwa taarifa potofu mtandaoni kuhusu masuala ya kifedha, zinakosa tija katika kujenga taifa na zinaweza kuhatarisha ustawi wa sekta ya fedha.
“Tunawaonya wote wanaoeneza upotoshaji huo mtandaoni kuacha mara moja, kwani taarifa hizo hazina tija katika maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa Tanzania kwa ujumla,” amesisitiza