DKT.NCHIMBI AOMBA KURA DODOMA MJINI, KESHO KUANZA KAMPENI MOROGORO

MGOMBEA Mwenza  wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema miongoni mwa mipango ya chama hicho kwa miaka mitano ijayo kikirudi tena madarakani ni kujenga Maktaba ya Taifa mkoani Dodoma.

Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo Oktoba 17, 2025, katika mkutano wake wa hadhara wa kampeni za CCM uliofanyika Wilaya ya Dodoma Mjini alipokuwa akimuombea kura mgombea urais wa chama chake Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea ubunge na udiwani ikiwa zimesalia siku 12 kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

“Maktaba hiyo itahifadhi kumbukumbu, nyaraka na maandiko mbalimbali ya kitaifa, na itatumiwa na watafiti, wanafunzi na wananchi kwa ujumla kwa maslahi ya taifa.”

Aidha Dkt.Nchimbi ameeleza kuwa Serikali ya  CCM pia imedhamiria kujenga shule mpya za msingi 21 na sekondari 16, madarasa 150, maabara 15 za sayansi na mabweni 17 ili kuboresha mazingira ya elimu na kupunguza msongamano darasani.

Hata hivyo baada ya kufanya mkutano wa kampeni katika Wilaya ya Dodoma Mjini, ikiwa ni mkutano wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi Mkuu katika Mkoa huo kesho Oktoba 18 Dkt.Nchimbi ataanza mikutano ya kampeni katika Mkoa wa Morogoro ambako ataomba kura za Mgombea Urais Dk.Samia pamoja na wagombea wengine wa Chama hicho.

Tangu kuanza kwa kampeni Dkt.Nchimbi amefanya mikutano ya kuomba kura za wagombea wa Chama hicho katika mikoa 24 na kote ambako amepita wananchi wamemuahidi kuwa CCM na wagombea wake wakiongozwa na mgombea Urais Dkt.Samia Suluhu Hassan watashinda kwa kura nyingi za heshima.