KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, amesema kufundishwa na Kocha, Mkongomani, Florent Ibenge ni hatua kubwa kwa timu hiyo kufikia malengo iliyojiwekea hasa michuano ya kimataifa.
Nyota huyo amezungumza hayo wakati kikosi cha Azam kikikabiliwa na mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya KMKM, itakayopigwa kesho Jumamosi Oktoba 18, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
“Ni motisha kwetu kama wachezaji lakini ni changamo pia kubwa iliyokuwa mbele yetu kufikia na kutimiza malengo yetu ambayo tumeyadhamiria kuyafikia pamoja msimu huu,” amesema Fei Toto.
Akiizungumzia KMKM, Fei Toto amesema anaamini itakuwa ni mechi ngumu kwa pande zote kutokana na miamba hiyo kujuana vyema kwani imeshakutana katika michuano mbalimbali.
“Tunaiheshimu KMKM kwa sababu ni timu nzuri lakini sisi kama wachezaji tumejipanga pia vizuri kuhakikisha tunatimiza azma ya kuingia hatua ya makundi, haitokuwa rahisi kwani zinapocheza timu za Bara na visiwani huwa ushindani unakuwa ni mkubwa,” amesema.
KMKM imefika raundi ya pili ya michuano ya CAF baada ya kuitoa AS Port ya Djibouti kwa jumla ya mabao 4-2, huku kwa upande wa Azam ikiitoa EL Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0.