Kagoma, Kante wamvuruga Pantev Simba, Rushine kubeba jukumu
KATI ya vitu vinavyompasua kichwa kocha Dimitar Pantev ambaye alitambulishwa kama meneja pale Msimbazi ni pamoja na eneo la kiungo mkabaji ambapo bado hajajua nani na nani wanatakiwa kuanza huku akiwa na machaguo manne kwenye kikosi hicho.
Licha ya kwamba Selemani Matola ndiye atakayesimamia shoo nzima kama kocha mkuu kutokana na kukidhi vigezo vya CAF, Mwanaspoti linajua kwamba Pantev anapambana kuona timu hiyo inafanya vyema na anaumiza kichwa huko Eswatini ambako timu hiyo Jumapili hii itakuwa uwanjani katika mechi yake ya kwanza ya ushindani kama meneja dhidi ya Nsingizini Hotspurs katika raundi ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Awali, Pantev huyo aliwatumia Mzamiru Yassin, Alassane Kante na kiraka Naby Camara katika mechi mbili za kimataifa za kirafiki dhidi ya Al-Hilal Omdurman ya Sudan lakini inaelezwa kwamba hakupata kile ambacho alikuwa akihitaji hasa katika mechi ya pili ambayo walipoteza kwa mabao 4-1. Mechi ya kwanza Simba ilishinda kwa mabao 2-1.

Katika mechi hizo, Simba ilikosa huduma ya baadhi ya wachezaji akiwamo Yusuph Kagoma ambaye alikuwa katika majukumu ya timu ya taifa la Tanzania ambayo ilikuwa Dubai kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Iran.
Urejeo wake kwenye kikosi hicho sambamba na wachezaji wengine kama vile, Morice Abraham, Wilson Nangu, Yakoub Suleiman na Seleman Mwalimu unaweza kuongeza kitu kwenye eneo hilo, ikumbukwe kuwa Kagoma ndiye aliyekuwa injini ya Simba eneo hilo msimu uliopita akicheza sambamba na Fabrice Ngoma ambaye aliondoka mwishoni.
Tangu kocha mkuu Fadlu Davids aondoke, Jumamosi Pantev alipata nafasi nzuri ya kufanya maandalizi ya mwisho akiwa na kikosi kamili hivyo atakuwa na nafasi nzuri ya kufanya uchaguzi juu ya nani kati ya viungo waliopo atacheza sambamba na Kagoma au ataamua kuendelea na wale ambao alikuwa nao katika maandalizi ya awali.

Katika mechi tano ambazo Simba imecheza za kimashindano ikiwamo moja ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, mbili za ligi na nyingine za kimataifa, wachezaji watano tofauti wametumika katika eneo hilo, akiwamo Abdulrazack Mohamed Hamza ambaye aliumia kwenye dabi.
Simba inahitaji uwiano wa uchezaji hasa katika mechi ya Jumapili hii ambapo watacheza ugenini ili kuwa na mwanzo mzuri na kwa mujibu wa taarifa inaelezwa kwamba kocha huyo amebaini udhaifu eneo hilo.
“Tunaweza kuona nini kitatokea kesho (leo) katika maandalizi yetu ya mwisho, unajua Pantev anataka viungo wenye uwezo wa kusaidia mshambulizi kwa haraka na kuzuia kwa pamoja, hakufurahishwa na kile ambacho kilitokea katika mechi ya pili dhidi ya Al Hilal,” kilisema chanzo.

Wakati akiondoka nchini kwa ajili ya kuifuata Nsingizini Hotspurs, Pantev alikuwa na matumani ya kufanya vizuri katika mechi hiyo; “Hatukuwa na wachezaji wote katika maandalizi yetu, ni kawaida hasa panapokuwa na kalenda ya FIFA, tutakuwa na programu ya pamoja na kuwa tayari kwa mechi, naamini tutafanya vizuri na kuingia makundi, lakini ni muhimu kwenda hatua kwa hatua, hatutakaa nyuma kuwasubiri.”
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa kwamba beki wa kati, Rushine De Reuck ambaye huu ni msimu wake wa kwanza akiichezea Simba, amependekezwa kuwa mmoja wa manahodha wa kikosi hicho.
De Reuck ambaye amefunga mabao mawili katika mechi mbili za ligi ni kati ya wachezaji ambao wanaonekana kuwa na sifa za uongozi hivyo Pantev anatajwa kumpendekeza raia huyo wa Afrika Kusini.

Mbali na mapendekezo hayo, bado Shomary Kapombe ataendelea kuwa nahodha mkuu na wakati atakaokosekana huenda akaonekana De Reuck akivaa kitambaa hicho cha unahodha, wachezaji wengine ambao watakuwa akionekana katika majukumu hayo ni pamoja na Mzamiru Yassin.