WAMEVUNJA mwiko. Hatimaye Pamba Jiji imepata ushindi wake wa kwanza msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa Mashujaa FC ya Kigoma kwa mabao 2-1.
Pamba imepata ushindi huo leo Oktoba 17, 2025 katika mchezo wa raundi ya nne ambao umechezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuanzia saa 8:00 mchana.
Mabao ya Pamba yamefungwa na mshambuliaji raia wa Uganda, Peter Lwasa mnamo dakika ya 16 kwa shuti akimalizia mpira ulioshindwa kuokolewa na mabeki.
Lwasa amefunga bao la pili dakika ya 62 kwa shuti akipokea pasi ya Najim Mussa, huku bao la Mashujaa FC likifungwa na Baraka Mtui katika dakika ya 45 kwa mpira wa moja kwa moja wa kutenga ambao umemshinda kipa Arijif Amour.
Lwasa aliyejiunga na Pamba msimu huu akitokea Kagera Sugar sasa anafikisha mabao matatu katika mechi tatu za Ligi Kuu, ambapo bao lingine alifunga katika sare ya bao 1-1 na Namungo FC kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Baada ya ushindi huo Pamba imefikisha pointi tano na kupaa hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, ikishinda mchezo mmoja, sare mbili na kupoteza mmoja, huku Mashujaa ikisaliwa na alama nne baada ya kupoteza mechi mbili, sare moja na kushinda moja.
Pamba imefuta rekodi mbaya ya msimu uliopita ambao ilicheza mechi saba za Ligi Kuu bila ushindi, huku ikicheza mechi tano za nyumbani bila kupata ushindi. Mchezo wa leo ni wa pili kucheza nyumbani ikipata ushindi na sare.
Huu ni mchezo wa tatu kwa timu hizo kukutana kwenye Ligi Kuu Bara tangu msimu uliopita, ambapo Mashujaa imeendeleza ubabe ikishinda 2-0 na sare ya mabao 2-2.
Katika mchezo huo, timu zote zimeshambuliana kwa zamu na kutengeneza nafasi kadhaa za mabao ambazo hata hivyo umakini wa washambuliaji ulikosekana. Mchezo huo pia haukuwa wa kasi kwani timu zote zimecheza kwa tahadhari na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Timu zote zimefanya mabadiliko, ambapo mapema dakika ya 45 Pamba ilimtoa James Mwashinga na kuingia Kenneth Kunambi, pia dakika ya Ibrahim Abraham, Najim Mussa na Peter Lwasa wamewapisha Abdallah Sebo, Mathew Tegis na Stephen Siwa dakika ya 77.
Mashujaa nao wamefanya mabadiliko ya wachezaji dakika ya 57 akitoka Ismail Mgunda na kumpisha Salum Kihimbwa, pia dakika ya 63 Mudhihir Vuai, Japhary Kibaya wamewapisha Crispin Ngushi na Daniel Lyanga.
Akizungumzia ushindi huo, Kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema umekuwa mzuri kwa kikosi chake kwani umeondoa hali ya kusemwa vibaya na mashabiki na sasa wataanza kujiamini.
”Hii ni furaha kwetu na imetupa nguvu, neno langu kwa mashabiki wasiniachie kazi pekee yangu watuunge mkono wawe nasi pamoja ili tushikamane tupate ushindi wa pili mchezo ujao,” amesema Baraza.
VIKOSI
Pamba Jiji: Arijif amour, Hassan Kibailo, Ibrahim Abraham, Abdulmajid Mangalo, Brian Eshianda, James Mwashinga, Zabona Mayombya, Kelvin Nashon, Yonta Camara, Najim Mussa na Peter Lwasa.
Mashujaa: Patrick Muntary, Baraka Mtui, Idrissa stambuli, Samwel onditi, Abdulnassir Assa, David Ulomi, Mpoki Mwakinyuke, Mundhir Vuai, Abdulmalik Zakaria, Ismail Mgunda na Jafary Kibaya.
Lwasa ang’ara Pamba Jiji ikivunja mwiko CCM Kirumba
