Dodoma. Ni kama vile Mahakama Kuu iliyosikiliza shauri la kikatiba lililofunguliwa na Luhaga Mpina na Bodi ya Wadhamini ya ACT-Wazalendo, imewaonyesha wadai hao mlango wanaoweza kupita kuendelea kudai haki yao.
Mpina na Bodi hiyo walifungua shauri la kikatiba dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kupinga hatua ya INEC kumwengua Mpina kugombea kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Hata hivyo, katika hukumu ya Oktoba 15, 2025, jopo la majaji watatu waliosikiliza shauri hilo, liliitupa kesi hiyo, likisema kwa maoni yao, shauri hilo lilipaswa kufunguliwa kwa njia ya mapitio ya mahakama (judicial review).
Mbali na uamuzi huo, majaji hao, Fredrick Manyanda, Sylvester Kainda na Abdallah Gonzi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma, walienda mbali na kusema kifungu cha sheria kilichokuwa kinalalamikiwa, hakijakiuka Katiba.
Hukumu hiyo ilitolewa zikiwa zimebaki siku 15 tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu unaovishirikisha vyama 17 vya siasa kikiwamo chama tawala (CCM), ambacho kimemsimamisha Samia Suluhu Hassan kugombea kiti cha Rais.
Katika hukumu, jopo hilo la majaji lilirejea kiini cha kufunguliwa kwa shauri hilo kuwa, Julai 29, 2025, mleta shauri wa kwanza (Mpina) alijiunga na chama cha mleta maombi wa pili na kupewa kadi ya uanachana namba ACT1005999.
Kwamba, Agosti 6, 2025, Mpina aliteuliwa na ACT-Wazalendo kupeperusha bendera yake kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Baadeye aliwasilisha maombi kwa INEC ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, akapewa fomu namba 8A ambayo aliijaza na kuirudisha INEC Septemba 13, 2025 lakini kabla ya kuteuliwa akakutana na pingamizi.
Moja ya mapingamizi matatu lilitoka kwa AG ambalo lilikubaliwa na INEC, hivyo kumwengua Mpina katika kinyang’anyiro hicho, ndipo aliamua kwenda mahakamani akipinga uamuzi huo pamoja na kifungu hicho cha 37(6).
Katika shauri hilo namba 24027/2025, Mpina na Bodi ya ACT-Wazalendo waliwakilishwa na mawakili John Seka, Edson Kilatu na Jasper Sabuni, wakati INEC na AG wakiwakilishwa na mawakili wakuu wa Serikali, Mark Mulwambo na Vivian Method.
Mawakili hao walisaidiwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Stanley Kalokola na Wakili wa Serikali, Elly Rumisha huku INEC ikiwa na mawakili watazamaji (watch brief) wawili ambao ni mawakili wakuu, Halima Mohamed na Catherine Gwaltu.
Shauri hilo la kikatiba kabla halijadikilizwa lilikutana na pingamizi kutoka INEC na AG.
Wajibu maombi hayo walieleza maombi ya madai hayawezi kutekelezeka na ni mabaya kisheria, kwani mahakama haina mamlaka kuhoji uamuzi wa INEC kulingana na kifungu cha 37(6) cha Sheria ya Uchaguzi ya Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.
Majaji walisema hakuna ubishi kuwa waleta maombi waliomba mambo mawili, moja ni mahakama itamke kuwa kifungu hicho cha 37(6) kinakiuka Katiba lakini pili, itamke kuwa uamuzi wa INEC kumwengua Mpina ulikuwa batili kisheria.
“Wajibu maombi walikuwa wazi sana kwamba, pingamizi lao la awali halihusu suala la Katiba au kifungu cha 37(6). Kwa hiyo ina maana hata kama lingefanikiwa, haliwezi kulifanya shauri zima likafikia kikomo,” inasema hukumu ya majaji.
Hii ni kwa sababu kuu mbili, kwamba pingamizi la awali limegusa seti moja tu bali inayohoji kifungu cha 37(6) haikuguswa na pingamizi, hivyo shauri linaweza kuendelea hata kama pingamizi la seti moja litakubaliwa na mahakama.
Hoja kuu ya mabishano ilikuwa ni kama mahakama inayo mamlaka ya kusikiliza shauri hilo ilihali kikiwapo kifungu cha 37(6) cha sheria ya uchaguzi, kikisomwa pamoja na Ibara ya 74(12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu 37(6) na Ibara ya 74(12) vinafanana kuwa hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na INEC katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya sheria na Katiba ya Nchi
Akiwasilisha hoja ya pingamizi, wakili Vivian Method alisema aya ya 2, 3, 4, 5, 6 na 7 ya viapo vya waleta shauri zinaonyesha wanapinga uamuzi wa INEC wa kumwondoa Mpina katika orodha ya wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2025.
Kulingana na wakili huyo, uamuzi huo hauwezi kuhojiwa na mahakama kulingana na masharti ya kifungu cha 37(6) na ibara ya 74(12) ya Katiba ya Tanzania.
Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, wakili Seka alisema katika shauri hilo, maombi yao waombaji hayahoji uhalali wa uamuzi wa mlalamikiwa wa kwanza (INEC), bali wanaiomba mahakama hiyo kutumia mamlaka yake ya asili ya usimamizi.
Wakili Seka alisema kuna uamuzi wa Mahakama ya Rufani yaliyosema Ibara ya 74(12) ya Katiba haiwezi kutafsiriwa ili kulinda matendo au matendo kinyume cha Katiba; au kinyume cha sheria au matendo ya INEC yasichunguzwe na mahakama.
Alienda mbali na kusisitiza kuwa kifungu cha 37(6) cha sheria ya uchaguzi hakiwezi kuwa sahihi dhidi ya uamuzi ambao ni batili na kusisitiza uamuzi wa INEC ni batili kisheria kwa sababu ulikiuka ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Tanzania.
Katika uamuzi wao majaji walisema mawakili wa upande wa waleta maombi walidai mahakama hii ina mamlaka yasiyo na kikomo na inaweza kuhoji uamuzi wa INEC kupitia mapitio ya mahakama au mapitio ya Katiba.
Mawakili wa serikali nao wanakiri kuwepo kwa mamlaka hayo lakini wanasisitiza kuwa kwa mujibu wa maneno ya wazi yaliyotumika katika kifungu cha 37(6) cha sheria ya uchaguzi, mamlaka hayo hayo yameondolewa waziwazi.
“Kama tunamwelewa vizuri Wakili Mkuu wa Serikali Method (Vivian), alimaanisha kuwa mahakama hii imezuiwa na kifungu cha sheria kilicholalamikiwa kuhoji uamuzi wa INEC ama kwa mantiki au kwa njia ya mapitio,” inasema sehemu ya hukumu ya majaji na kuongeza:
“Tunakubaliana naye katika pendekezo la kwanza kwamba mahakama hii izuiwe kuhoji uhalali wa uamuzi wa INEC. Mantiki haiko mbali. Ni kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafikia mwisho.”
“Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba mamlaka ya urithi yasiyokuwa na vikwazo ya mahakama hii iliyopewa na ibara ya 107A, 107B na 108(2) ya Katiba ya Tanzania ya 1977 ya kuhoji uhalali wa kifungu kinachopingwa pia yameondolewa,” wamesema majaji na kuongeza:
“Kwa hivyo hatukubaliani naye kuhusiana na pendekezo la pili kwamba mahakama hii haina mamlaka hata kidogo ya kuchunguza uhalali au vinginevyo uamuzi wa INEC.”
Majaji wameongeza: “Tunasema hivyo kwa sababu mahakama hii haiwezi kuona dhuluma inayoonekana na kukaa tu kutazama, inalazimika kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba malengo ya Katiba yaliyoainishwa chini ya ibara husika zinazolinda amani na utulivu kama ilivyoelezwa katika ibara ya 9 ya Katiba yanatekelezwa.”
Majaji walinukuu msimamo wa Mahakama ya Rufani unaoelezea mapitio ya mahakama kwamba ndiyo silaha muhimu mikononi mwa majaji wa Tanzania ambayo raia wa kawaida anaweza kutumia kupinga uamuzi kandamizi.
“Tunafahamu kuwa jambo lililo mbele yetu si mwaliko wa mapitio ya mahakama bali ni mapitio ya Katiba, ambayo kwa kuangalia nafuu inayotafutwa ni dhahiri kwamba waleta maombi wanahoji uamuzi wa INEC ambao ungeweza kufanywa kupitia mapitio ya mahakama,” wamesema majaji na kuongeza:
“Kama tulivyoeleza, waleta maombi walijibu pingamizi hilo kwa kueleza kuwa maombi yao hayahoji uhalali wa uamuzi wa INEC, lakini wakati huohuo tunashangaa kwa nini hawakuomba mapitio ya mahakama kuhusu malalamiko katika suala hili, ili mahakama hii iweze kutumia vitendea kazi vyake?”
Mathalan, majaji hao walisema waombaji wanasema sababu ya kubisha hodi katika mlango wa mahakama ni INEC kumwengua Mpina na kwamba, haikuwa kosa la kawaida bali kukiuka haki ya asili ya mgombea.
“Tuna maoni kwamba malalamiko kama hayo yana msingi mzuri wa mapitio ya mahakama, mchakato ambao haujajumuishwa na kifungu cha 37(6)” wamesema.
Majaji wamesema badala yake, waleta shauri hawasafiri katika mrengo huo na badala yake wanahoji uhalali wa INEC ambao unakatazwa na kifungu hicho.
Katika hitimisho la jumla, majaji walisema wanaona kifungu cha 37(6) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani hakijavunja Katiba, na kinaweza kuhojiwa na mahakama kupitia mapitio ya mahakama.