Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato Kusini(Kushoto) akizungumza na mawakala wa usafirishaji stendi ya mabasi Buseresere na kulia ni mgombea Udiwani wa kata hiyo,Mange Samwel.
…………………
CHATO
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chato kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Paschal Lutandula, amewatembelea wafanyabiashara wa soko la nafaka na chakula kwenye mji mdogo wa Buseresere wilayani Chato kisha kuwaomba kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.
Mgombea huyo aliyeambatana na mwenyekiti wa Jumuia ya wananwake wa CCM ( UWT) mkoa wa Geita, Rolensia Bukwimba, wamelazimika kuwasalimia wafanyabiashara hao kabla ya kushiriki mkutano wa kampeni za Urais,Ubunge na Udiwani kwenye Kijiji cha Ibondo kata ya Buseresere.
Mbali na hilo, mgombea huyo amewatembelea mawakala wa usafirishaji abiria kwenye stendi ya mabasi Buseresere kisha kuwaahidi kushirikiana nao katika kuboresha sekta ya usafirishaji kwa madai kuwa changamoto zao anazifahamu na kwamba zitakwenda kutatuliwa iwapo watamchagua kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.
“Ndugu zangu wananchi na wafanyabiashara wa hapa Buseresere ninawaomba sana kura zenu, pia ninamiombea kura nyingi mgombea Urais wa CCM, mama yetu mpendwa Dkt. Samia pamoja na mgombea udiwani wa Kata ya hii, Mange Samwel ili tushirikiane kwa pamoja kuwaleteeni maendeleo” amesema Lutandula.
Kadhalika amekazia kauli yake ya kuubadili mji wa Buseresere kuwa Dubai ya Tanzania kutokana na uwepo wa wafanyabiashara wakubwa na wadogo ambao hutamani kufanya kazi usiku na mchana kwa lengo la kuinua uchumi wao kwa wepesi zaidi.
Awali mgombea huyo, ameshuhudia kupokelewa kwa baadhi ya wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) ambao kwa hiari yao wameamua kujiunga na CCM kwa madai ya kuridhishwa na kazi nzuri zilizotekelezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni mgombea Urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza na baadhi ya wana CCM walioshiriki kuwapokea wafuasi hao wa Chadema, aliyekuwa Katibu wa Chadema tawi la Mapinduzi, Shija Erasto, pamoja na Sahani Joseph, wamesema wamewiwa kurejea CCM baada ya kufurahishwa na mipango thabiti ya maendeleo inayotekelezwa na Chama hicho.
Aidha Erasto amedai kuwa anayo imani kubwa ya maendeleo ya kweli kwenye mji wa Buseresere kutokana na CCM kumteua,Paschal Lutandula, kupeperusha bendera ya Ubunge kupitia CCM, kwa madai ni mtu sahihi mwenye maono na nia njema ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwisho.