Mgombea urais wa DP kutoa matibabu, chakula bure kwa wanawake na watoto

Lindi. Mgombea urais kupitia Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Mluya, ameahidi kuwa endapo atapata ridhaa ya kuingia madarakani, serikali yake itahakikisha wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu wanapata matibabu bure huku akinadi mpango wa kuwapatia chakula bure wanawake wanaotoka kujifungua ndani ya miezi mitatu ya kwanza.

Mluya ametoa ahadi hizo leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, wakati akihutubia wananchi wa eneo la Mnazi Mmoja, Jimbo la Lindi Mjini, katika mkutano huo wa kampeni aliwaomba wananchi kumpa kura ili alete mabadiliko yenye kugusa maisha ya watu wa kawaida.

“Nikiingia madarakani, nitahakikisha wanawake wanaotoka kujifungua wanapata chakula bure kwa miezi mitatu. Pia sitaki kuona maiti zikichajiwa fedha hospitalini. Wazee, watoto na watu wenye ulemavu watapata matibabu bure. Serikali yangu itahakikisha huduma za kijamii zinakuwa za huruma na utu,” amesema Mluya.

Akiendelea na hotuba yake, mgombea huyo wa urais amesema serikali ya DP itajikita zaidi katika kuzalisha ajira kupitia kilimo, kurejesha viwanda na kuboresha mitaala ya elimu ili iendane na mahitaji ya soko la ajira la sasa.

“Tutaboresha mitaala ya elimu ili iwe ya vitendo zaidi, na tutaacha kutegemea mikopo ya nje. Lazima tuwe taifa linalojitegemea kiuchumi. Pia tutaondoa kikokotoo cha pensheni kinacholalamikiwa na wastaafu, kuongeza mishahara ya watumishi wa umma, na kuboresha makazi ya askari,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Lindi Mjini kupitia DP, Tulibu Mkononi, amesema akipewa nafasi ya kuongoza, ataweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya elimu, kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na kutatua changamoto zinazoukabili mkoa huo.

“Nitapambana kuhakikisha shule zina miundombinu bora, walimu wanapata vifaa vya kufundishia na wanafunzi wanasoma katika mazingira salama. Changamoto zote za Lindi Mjini nitazitatua kwa vitendo, si maneno,” amesema Mkononi.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walionesha kuvutiwa na sera za DP, lakini wakasisitiza umuhimu wa utekelezaji endapo chama hicho kitapata nafasi ya kuongoza.

Saada Omary, mkazi wa Mnazi Mmoja, amesema sera zilizotolewa na wagombea hao zina mwelekeo mzuri wa kuleta maendeleo kwa mkoa wa Lindi, lakini akasisitiza kuwa hazipaswi kuishia kwenye majukwaa.

“Sera za DP ni nzuri sana, hasa kuhusu huduma za afya bure na kuboresha elimu. Lakini wasije wakaishia kusema maneno matamu kwenye majukwaa. Wakipewa ridhaa, wazitekeleze kwa vitendo,” amesema.