Mgombea wa NCCR aomba kura za CCM

Musoma. Mgombea urais kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, Haji Hamisi amewataka Watanzania wakiwemo wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwapigia kura wagombea wa chama chake katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, ili kuleta mabadiliko ya kiuongozi na maendeleo ya kiuchumi nchini.

Hamisi ametoa wito huo leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, wakati akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Machinjioni, mjini Musoma. Alisema chama chake kinawajali na kuwathamini wananchi zaidi kuliko chama kilicho madarakani.

“Sisi tunawaheshimu ninyi, hata kwa huu uchache wenu. Tofauti na kule kwingine ambako wananchi hawaheshimiki. Kama wangekuwa wanaheshimika, basi kero zao zingesikilizwa na kutatuliwa. Mkitupa ridhaa, tutahakikisha tunaziondoa kero zote kwa sababu tunawathamini Watanzania,” amesema Hamisi.

Ameongeza kuwa Watanzania wamefika hatua ya kufanya mabadiliko ya kweli ya uongozi kwa kumchagua kiongozi na chama kipya kitakachosikiliza na kuhudumia wananchi, akisisitiza kwamba chama hicho ni NCCR-Mageuzi.

Hamisi amesema baada ya kufika Musoma, amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wakazi wa mji huo, ikiwemo kuhusu uuzaji wa maeneo ya wazi na utoaji holela wa vibali vya ujenzi katika maeneo yasiyoruhusiwa.

“Hili suala la kuuza maeneo ya wazi na kutoa vibali vya ujenzi kinyume cha sheria tutalishughulikia. Hata kama hatutapata ridhaa ya kuongoza nchi, nitahakikisha wanasheria wetu wanalifuatilia na waliohusika wanapelekwa mahakamani. Hatuna mzaha katika hili,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa Watanzania wenye sifa kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi, akiwataka wasiwe na hofu kwani uchaguzi utakuwa wa amani.

“Kupiga kura ni haki ya kikatiba. Msisikilize wanaohamasisha msipige kura. Jitokezeni kwa wingi Oktoba 29, mchague viongozi mnaowaamini. Kwa sera tulizonazo, naamini mtaamua kutupa nafasi ya kuwatumikia kwa miaka mitano ijayo,” amesema.

Hamisi amesisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuwa na ajenda moja tu kuiondoa CCM madarakani kupitia sanduku la kura.

“Mabadiliko hayawezi kutokea kama hamtapiga kura. Kila mmoja ana wajibu wa kushiriki katika mabadiliko haya. Mkishapiga kura, rudini nyumbani muendelee na shughuli zenu. Hakutakuwa na wizi wa kura; tumejipanga kuhakikisha kila kura inahesabiwa ipasavyo,” amesema huku akiwataka polisi kutojihusisha na vitendo vya wizi wa kura.

Katika mkutano huo, baadhi ya wagombea udiwani wa NCCR-Mageuzi katika Manispaa ya Musoma pia walipata nafasi ya kueleza sera zao.

Mgombea wa Kata ya Rwamlimi, Nyang’era Gogo, amesema endapo atachaguliwa, atahakikisha anatafuta suluhisho la kudumu kwa tatizo la mafuriko ambalo limekuwa likisababisha maafa na umasikini kwa wakazi wa eneo hilo.

“Chanzo kikuu cha mafuriko ni miundombinu mibovu na ujenzi holela kwenye mikondo ya maji. Nikichaguliwa, nitahakikisha tatizo hili linamalizika na wale waliopoteza mali kutokana na mafuriko wanapata fidia,” amesema Gogo.

Kwa upande wake, mgombea wa Kata ya Mshikamano amesema eneo hilo limekuwa nyuma kimaendeleo kutokana na ukosefu wa viongozi wenye maono.

“Nikipewa nafasi, nitahakikisha kata yetu inapiga hatua kimaendeleo ya watu na vitu. Hatuna sababu ya kubaki nyuma; tunachohitaji ni uongozi wenye dira na nia ya dhati,” amesema.