Mke mbaroni kwa tuhuma kumuua mumewe na kumzika chumbani

Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia Martha Japhet (44), mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Mzalendo, Kijiji cha Mawemeru, Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita, kwa tuhuma za mauaji ya mumewe, Shabani Paschal (55), ambaye pia alikuwa mkulima na mchimbaji wa madini.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Safia Jongo, kupitia mitandao ya kijamii ya jeshi hilo, imeeleza kuwa tukio hilo limegundulika baada ya marehemu kutorudi nyumbani kwa zaidi ya siku tano.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa Oktoba 16, 2025, saa 1:00 asubuhi, kuhusu kutoweka kwa Shabani Paschal tangu Oktoba 11, 2025, saa 3:00 usiku, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa uchunguzi wa kina.

“Baada ya uchunguzi wa awali kufanyika, majira ya saa saba mchana siku hiyo hiyo ya Oktoba 16 tulibaini uwepo wa mauaji hayo, na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Martha Japhet kwa mahojiano,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kamanda Jongo amedai kuwa, mtuhumiwa huyo alieleza kumpiga mumewe kichwani kwa kutumia kitu chenye ncha kali, hatua iliyosababisha kifo chake papo hapo.

Inadaiwa mtuhumiwa alichimba shimo ndani ya chumba walichokuwa wakilala, kisha akamzika marehemu humo humo na kujaza kifusi cha udongo, kabla ya kufunika sehemu hiyo kwa magunia ya mihogo (udaga) ili kuficha ushahidi.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio ni migogoro ya kifamilia. Uchunguzi unaendelea, na pindi utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili,” imeongeza taarifa ya Polisi.

Kamanda Jongo amewataka wananchi wa Mkoa wa Geita na Watanzania kwa ujumla kuepuka kujichukulia sheria mikononi na badala yake kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya dola endapo wataona viashiria vya migogoro au vitendo vya ukatili katika jamii.

“Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kali kwa wote watakaobainika kujihusisha na matukio ya kihalifu, hususani mauaji ndani ya jamii,” amesema Kamanda Jongo.