Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imetangaza kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi ambapo sasa itakuwa ni Sh358,322 kutoka Sh275,060 ikiwa ni ongezeko la asilimia 33.4.
Kima hicho kitaanza kutumika rasmi Januari Mosi mwaka 2026. Ikumbukwe Serikali ilipandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 (kutoka Sh370,000 hadi Sh500,000), kwa lengo la kuimarisha ustawi kwa wafanyakazi.
Hilo likitangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa (Mei Mosi) mkoani Singida katika viwanja vya Bombadia, Mei mwaka huu.
Akitangaza kima hicho cha sekta binafsi leo Ijumaa Oktoba 17, 2025 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete kuongezwa kwa kima cha mshahara ni takwa la kisheria.
Amesema tangazo la mara ya mwisho lilikuwa mwaka 2022 hivyo tangazo la leo mwaka 2025 imetimia miaka mitatu. Sheria inataka kila baada ya miaka mitatu kufanyike mapitio ya kima cha chini cha mshahara.
“Nitoe rai kwa waajiri wote wa sekta binafsi kuzingatia na kutekeleza kima hiki kipya cha mshahara kwa kuwa ni takwa la kisheria. Ofisi yangu haitasita kuchukua hatua kwa waajiri watakaokaidi au kushindwa kitekeleza amri hii kwa makusudi.
“Aidha ofisi yangu itaendelea kufatilia kwa karibu utekelezaji wa amri hii, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi pamoja na kufanya tathimini ya mara kwa mara ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kikamilifu,” amesema.