KIUFUPI alikuwa anajipenda. Na kwa jinsi alivyokipenda chumba chake, haitakuwa ajabu unapoisikia stori yake ikakujia kumbukumbu ya wimbo ‘Ghetto Langu’ wa Ngwair.
“Haya ndio maisha, sio kufikiria kwenda Ulaya…hapa sasa utafute mke uoe…” alisema mama yake Bi Faudhia bila ya kujua akilini mwa mwanaye alikuwa akifikiria nini.
Wazazi wake walidhani Muddy alikuwa ameridhika na maisha ya kufanya kazi kama dereva wa teski wakaamini hayo ndio yangekuwa maisha yake ya kila siku, hawakujua mtoto wao alikuwa akifikiria nini kuhusu maisha yake ya baadaye.
Ndotoni mwake bado kulikuwa na safari ya Ulaya, hakufikiria kabisa kufunga ndoa na mwanamke yeyote wa Kitanzania, ndoto yake ilikuwa ni kuoa mwanamke wa Kizungu.
***
BAADA ya kutuliza akili, mfanyabiashara wa Kicongomani Kamba hakuwa na kufanya zaidi ya kumkumbuka dereva wake wa zamani.
Pamoja na kitendo kilichomuudhi alichofanyiwa na dereva huyo Kamba hakuwa na budi kusahau na kurudisha imani kwake. Aliamimi laiti kama asingechukua uamuzi wa hasira na kuamua kumsubiri dereva wake wa siku zote, Mmaka, asingepoteza pesa na mali zake.
Hivyo, dereva wake wa zamani, alikuwa ndiye mtu muhimu kwake kwa wakati huo kuliko wakati mwingine wowote ule, alimpigia simu na kumwambia amfuate Kariakoo.
“Kuna nini bosi?”
“Wee ukuje tu…” alisema Kamba kwa sauti iliyojaa uchovu akikwepa kumhadithia kila kitu kwenye simu. Muda wote Kamba alipata hifadhi katika duka ambalo awali aliingia mara ya mwisho kununua bidhaa.
Ilikuwa ni baada ya kurudi ndani na duka hilo akiwa na bidhaa alizozinunua huku akiwa ametahayari kiasi cha kuwashtua wauzaji wa duka hilo.
“Vipi, kuna tatizo?” Mmoja kati ya wahudumu wa duka hilo alimuuliza Kamba baada ya kumuona akiingia dukani humo akiwa katika hali ya kukata tamaa.
Hapo ndipo Kamba alipoanza kuwahadithia mkasa mzima uliomkuta na kuwafanya wauzaji wa duka hilo pamoja na baadhi ya wateja waliokuwamo ndani kushangazwa na tukio hilo.
“Dereva humjui kabisa?” mhudumu mwingine wa duka hilo alimhoji Kamba.
“Mi hapana kujua yeye kabisa…”
“Hata namba ya gari hukuishika?”
“Hamna kabisa, ndio kwanza naona yeye leo.”
“Ulimpata kwenye mtandao?” mteja mwingine wa duka hilo alimuuliza ili kutaka kumsaidia Kamba namna ya kuweza kumtambua.
“Hapana, alikuja tu hotelini na mgeni mwingine nikamchukua…” alijibu kinyonge.
“Itabidi uripoti polisi…” alishauri mhudumu wa duka hilo.
Baada ya muda, Mmaka dereva aliyekuwa akitumiwa na Kamba katika shughuli zake alipiga simu na kumwambia alikuwa amefika Mtaa wa Tandamti.
Kamba alitoka nje ya duka na kumuelekeza sehemu aliyokuwapo. Dereva alipofika alimuona bosi wake hakuwa katika hali yake ya kawaida. Alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.
“Vipi wamekupiga nini?” alimuuliza Kamba lakini Mkongomani huyo hakuielewa lugha hiyo ya watoto wa mjini.
“Nimeibiwa…” Hapo ndipo Kamba alipoanza kumsimulia mkasa mzima dereva wake.
Dereva huyo alitamani kucheka kutokana na Kamba kumuacha, lakini nafsi yake ilimsuta baada ya kugundua yeye ndiye aliyekuwa chanzo cha tukio hilo zima.
Ni kutokana na kushindwa kumwambia ukweli tajiri yake huyo kwamba angechelewa kumfuata hotelini asubuhi ya siku hiyo wakati walipokuwa wakiwasiliana.
“Dah! Pole sana umesharipoti polisi?” Mmaka alimuuliza.
“Bado, ndio maana nimekuita wewe unisaidie kufuata utaratibu wote,” alisema Kamba kwa unyonge.
Dereve huyo akamsaidia Kamba kwenda kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Msimbazi na Kamba alihojiwa kuhusiana na tukio hilo naye akatoa maelezo yote.
Kamba hakuweza kukumbuka vitu vingi alivyoulizwa na askari wa upelelezi zaidi ya aina ya gari na rangi yake. Lakini hakulijua jina la dereva wala hakuwahi kuishika namba ya gari.
***
MARA baada ya kufanikiwa kumtoroka Kamba katika mitaa ya Kariakoo, Muddy aliendesha gari kwa kasi hadi mitaa ya gerezani.
Kwanza aliingia nyumbani kwao na kila mmoja alishangaa kutokana na kasi alioingia nayo. Ni kama mtu aliyekuwa anafukuzwa.
Moja kwa moja, Muddy aliingia chumbani kwake na kuchukua begi lake la nguo na alihakikisha hati yake ya kusafiria ilikuwa ndani ya begi hilo dogo.
Kama alivyoingia, ndivyo alivyotoka kiasi hata cha kusahau kuufunga mlango wa chumba chake. Mama yake aliyekuwa ukumbini alishangazwa na kasi ya aliyoingia na kutoka nayo mwanaye. Muddy akiwa na haraka moja kwa moja aliendesha gari hadi masikani kwao ambako alikuwa akipenda kushinda kipindi alipokuwa hana kazi.
Muddy alimfuata rafiki yake, Hamisi Sungajao aliyemkuta katika ghetto la wavuta bangi katika kitongoji hicho cha Gerezani.
“Kamanda njoo haraka…” alisema Muddy akimtoa rafiki yake katikati ya kundi la vijana wengine huku akitaka watu waliokuwapo katika genge hilo wasijue kilichokuwa kinaendelea.
Walipofika nje, wakaingia ndani ya gari na Muddy akaiondoa gari katika eneo lililokuwa na macho ya watu wengi na kwenda kuligesha mbali kidogo.
Akiwa na haraka, Muddy akachomoa kiasi cha pesa za Kitanzania na kumpatia Hamisi. Zilikuwa pesa nyingi kiasi cha kumtia kiwewe rafiki yake huyo.
“Hizi pesa za nini?” Hamis alihoji huku akimwangalia rafiki yake.
“Subiri kwanza…” alisema Muddy aliyekuwa akitafuta vitu vingine vya Kamba Makambo na kumkabidhi Hamisi.
“Umepata wapi hivi?” Hamisi aliendelea kuhoji.
“Kuna ng’ombe ameingia ndani ya kumi na nane zangu nikamchinja…,” alisema Muddy huku Hamisi akiwa haamini alichokuwa akikiona wala kukisikia.
“Shika hizo pesa, kuanzia kesho asubuhi anza mchakato wa kutafuta passport ya muda mfupi, nitakusubiri Nairobi…”
Baada ya kusema maneno hayo, Muddy akamweleza kwa kifupi rafiki yake tukio zima lilivyotokea, alianza kumwambia jinsi alivyokutana na Kamba na alivyomalizana naye katika mitaa ya Kariakoo.
Muddy alimwambia Hamisi baadhi ya vitu ambavyo Kamba alikuwa amevinunua avipige bei na kuweza kuongezea pesa za kumfikisha Nairobi na vingine anaweza kuvitumia.
“Usimwambie mtu yeyote kuhusu ishu hii, changamkia passport uwezavyo keshokutwa tukutane Nairobi kwa Fashanu hapo tutazungumza kwa kina …” alimalizia Muddy.
Hapo Hamisi ndio kama alikuwa anazinduka kutokana na bangi alizokuwa amevuta na akaanza kumuelewa rafiki yake, akili yake ikafunguka, akajua tayari kumekucha.
Wakaagana na Muddy aliondoka na gari kwa kushika njia ya kwenda Mnazi Mmoja, akapita Faya, Magomeni, Manzese, Ubungo, Kimara na Mbezi… Kibamba, Kibaha hatimaye akafika Kongowe mkoani Pwani, akaingia katika katika njia ya mchepuko.
Baada wa mwendo kama dakika kumi hivi akaliona shamba moja lililokuwa limepaliliwa vizuri hapo ndipo alipoamua kulitelekeza gari hilo.
Kabla ya kufanya hivyo alihakikisha amechukua kila kitu kilichokuwa na umuhimu kutoka kwenye gari na briefcase ya Kamba Makambo na kuachana na vile ambavyo havikuwa na umuhimu wowote kwenye safari yake.
Pia, aliweka vizuri kila kitu chake alichokihitaji katika safari yake ya maisha iliyokuwa ikianza rasmi kutoka hapo.
***
MZEE Mangushi ndio kwanza alikuwa amemaliza kujiandaa na alikuwa akisubiri kupatiwa kifungua kinywa na mkewa Bi Swabra ili aende kwenye shughuli zake.
Hii imekuwa desturi yake karibu kila siku, kabla ya kutoka nyumbani alikuwa akiandaliwa kahawa na mkewe, ambapo hunywa vikombe vyake vitatu kisha huenda kwenye shuguli zake na akirudi saa nne ndipo alipokuwa akinywa chai.
Tayari alishaketi kwenye kiti chake cha kunesanesa sebuleni akiangalia habari kupitia runinga akimsubiri mkewe amletee birika na kikombe cha kahawa, ghafla alishtushwa na kengele ya mlangoni iliyoashiria kulikuwa na ugeni nje ya nyumba yake.
Mawazo yakamtuma ni Muddy ndiye aliyekuwa akija kuleta hesabu za gari. Kijana huyo aliyemkabidhi gari yake hakuwa ameleta hesabu kwa siku mbili.
Mzee Mangushi hakuwa na wasiwasi na kitendo hicho cha Muddy na hii haikuwa mara yake ya kwanza kufanya hivyo, kuna wakati biashara huwa inakuwa ngumu na alikuwa akipitisha siku mbili hadi tatu ndipo humpelekea malipo yake.
Kitu kingine kilichomfanya asiwe na wasiwasi na kijana huyo ni kutokana kuwa ni mtoto wa swahiba yake, mzee Tuesday Manyara.
Wazee hao, walikuwa na umri unaokaribiana na wameishi jirani katika maeneo ya Gerezani kwa muda mrefu sana. Wakati ambapo mzee Manyara akiwa ni mfanyakazi aliyeajiriwa serikalini na mzee Mangushi akiwa ni mfanyabiashara akimiliki maduka yake katika kitongoji hicho cha Gerezani.
“Karibuuu…” mzee Mangushi alimkaribisha mtu aliyekuwa akigonga kengele, mawazo yake bado yalikuwa yakiamini ni Muddy ndiye aliyekuwa akigonga.
Lakini kengele ilivyokuwa ikiendelea kugongwa akafuta imani yake kwamba aliyekuwa akigonga hakuwa kijana huyo, kwa sababu Muddy alikuwa mwenyeji sana ndani ya nyumba hiyo, alipokaribishwa mara moja tu aliingia, sasa aliamini kulikuwa na mgeni mwingine ambaye hakuwa Muddy.
Akanyanyuka na kuufuata mlango kutaka kumjua mtu aliyekuwa akigonga, mara baada ya kuufungua mlango alikutana na sura mbili ngeni machoni pake. “Shikamoo mzee…” vijana wawili wa kiume walijikuta wakitoa salam kwa zamu mara tu baada ya mzee Mangushi alipofungua mlango na kutoa uso wake nje.
Mtoto wa Mjini – 5
