:::::::::::
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza mwelekeo
wa mvua za msimu wa Novemba 2025 hadi Aprili 2026 kwa maeneo yanayopata msimu
mmoja wa mvua kwa mwaka, ikidai kuwa msimu huo utatawaliwa na vipindi virefu
vya ukavu pamoja na mtawanyiko wa mvua usioridhisha katika maeneo mengi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa
(IPCC), amesema mvua zinatarajiwa kuanza mwezi Novemba na kumalizika kati ya Aprili
na Mei 2026, lakini hazitakuwa za kuridhisha katika maeneo mengi.
Maeneo yanayotarajiwa kuathirika ni pamoja na mikoa ya magharibi (Kigoma,
Tabora, Katavi), kanda ya kati (Singida, Dodoma), nyanda za juu kusini
magharibi (Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa), kusini (Ruvuma), ukanda wa
pwani ya kusini (Lindi, Mtwara), pamoja na kusini mwa Morogoro.
Amesema mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya
mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei 2026 katika maeneo mengi yanayopata
mvua za msimu.
Dk. Chang’a amesema ongezeko la mvua linatarajiwa katika
kipindi cha nusu ya pili ya
msimu unaonza mwezi Februari mpaka Aprili, 2026
ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya mwezi Novemba, 2025 mpaka Januari, 2026.
Pamoja na mvua hizo kuwa za wastani hadi chini ya wastani,
Dk. Chang’a ametoa angalizo uwepo wa matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza
kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.
Dk. Chang’a amewashauri wadau kufuatilia taarifa
za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari kama zinavyotolewa na Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili waweze kujua mabadiliko yanayotokea katika
mifumo ya hali ya hewa kwa kila siku.