OMO aahidi kukomesha ufisadi taasisi nne Zanzibar ndani ya siku 100

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema akitangazwa kuwa rais wa kisiwa hicho, atafukua makaburi ili kushughulikia kile alichodai ni ubadhirifu wa uendeshaji katika taasisi nne.

Taasisi hizo ni moja Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa), Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) na Wizara ya Afya.

Katika maelezo yake, Othman amesema hajaridhishwa na mwenendo wa uendeshaji wa taasisi hizo za Serikali, akidai sheria ya utumishi wa umma umekiukwa na kutoa mwanya wa ubadhirifu wa fedha za umma.

Othman ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 17, 2025 akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Garagara Jimbo la Mwera Mjini Unguja, akitokea Pemba baada ya kuhitimisha ziara ya kampeni kwa awamu ya tatu kisiwani humo.

Kabla ya kutoa msimamo huo, Othman amesema dunia kote hakuna nchi iliyopiga hatua kama hakuna utumishi wa umma uliokuwa madhubuti.

“Wenzetu Singapore ambao ni mfano wa dunia wa maajabu ya maendeleo, kisiwani kidgo lakini leo kina uchumi unaozidi Malaysia. Singapore ni kisiwa kidogo hata Pemba kubwa,” amesema.

“Uchumi wao ni mkubwa sana, alipoulizwa Waziri Mkuu Singapore nini siri yao akajibu ‘Serikali yenye uadilifu maana ya utumishi wa umma’. Mojawapo ya misingi ya utumishi wa uhuru wa mamlaka zilizoanzishwa kisheria, lakini hali ya sasa visiwani humo na miaka ya nyuma,”amesema.

Othman amesema mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar ipo kisheria lakini uendeshaji wake, hauridhishi akidai unakwenda kinyume cha sheria na misingi ya utumishi wa umma ikiwemo utoaji wa zabuni za miradi.

“Inshalllah baada ya Oktoba 29 kaburi la mwanzo nitakalopeleka greda lifukuliwe ni mamlaka ya viwanja vya ndege, kwa sababu sheria za utumishi wa umma zimewekwa pembeni.

“Pia Zeco itakuwa kaburi la pili, nako nitafukua kuhusu uendeshaji kuna shida huko. Zawa ni taasisi iliyoanzishwa kisheria, lakini imewekwa pembeni, watu wametafutwa wao wanaowataka ili kuwapa zabuni…,” amedai.

Othman ameongeza kuwa, “Kabuli kubwa litakalofukuliwa amepewa Mazrui kulinda (Nassor Ahmed- Waziri wa Afya na mgombea uwakilishi Jimbo la Mwera- ACT Wazalendo. Hapa kuna malalamiko makubwa kuhusu utoaji wa zabuni kwa kampuni kusimamia hospitali.

“Kampuni za kuleta dawa na vyakula, zimechukuliwa na wenyewe. Haya mambo haya nitakwenda kuyahamisha na kuyatafutia mahali pa kukaa ili kurudisha utumishi wa umma, ndani ya siku 100,” amesema Othman.

Othman amesema Zanzibar inapoumwa panajulikana kikubwa Wazanzibari wampe imani ya kumchagua kwa kishindo ili akatoe tiba ya kisiwa hicho kwa sababu dawa anayo.

“Wala siingii maabara dawa ninazo kwenye mkoba, nasubiri kuingia wodini kuanza kazi. Nitarekebisha mfumo wa utumishi wa umma, nitahakikisha ninawapa maslahi yanayofanana, kikubwa nipeni funguo (kura),” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amewataka wananchi wa Mwera, kumchagua kwa kura za kishindo mgombea uwakilishi wa jimbo hilo, Mazrui.

“Tumewaletea mgombea chuma cha pua, Nassor Ahmed Mazrui, ndio maana mnasikia Dk Hussein Mwinyi akimsifia kutokana na utendaji kazi wake,” amesema.

“Mazrui amefanya kazi kubwa hapa kipindi jimbo hili linaitwa Mtopepo, hadi leo neema zake zinaonekana,” amesema Jussa ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi ya Wazalendo, Zanzibar.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, mkoa wa kichama wa Magharibi A Unguja, Raisa Bakari amesema chama hicho, kimejipanga vizuri kunyakua majimbo yote matano yaliyopo katika mkoa huo.

“Hatuna wasiwasi kabisa na ushindi wa majimbo yote Matano, naamini kwa uwezo wa Mungu tutashinda tena kwa furaha,” amesema Rais akifungua mkutano huo wa kampeni za Othman.